Michael Dalali
7 min readMar 26, 2019

--

Adhimisho la Misa Takatifu na Huruma ya Mungu

Sakramenti ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristu ni sakramenti kuu kuliko sakramenti zote kwani ndipo alimo Yesu Kristu mwenyewe mzima; Mwili wake, Damu yake, Umungu wake katika maumbo ya mkate na divai.

Sakramenti hii imewekwa na Kristu mwenyewe wakati wa karamu ya mwisho (Luka 22 :14–20). Kwa njia ya makuhani, Sakramenti hii hufanyika katika adhimisho la Misa takatifu. Tufahamu kuwa, bila Misa hakuna Ekaristi Takatifu na bila Padre hakuna Misa kwani hiyo itaishia kuwa ibada tu. Padre anasimama kwa niaba ya Yesu Kristu mwenyewe katika kuadhimisha fumbo la imani; yaani Padre anakuwa Kristu ‘impersona Christi’.

“Ekaristi Takatifu ndiyo moyo na kilele cha uzima wa Kanisa, kwani ndani yake Kristu hulishirikisha Kanisa lake na viungo vyake vyote na sadaka yake ya sifa na shukrani iliyotolewa msalabani kwa Baba yake mara moja kwa daima. Kwa njia ya sadaka hii, anamimina neema za wokovu juu ya mwili wake, ndilo Kanisa” (KKK, uk 336)

Tunaweza kujiuliza; Kuna uhusiano gani kati ya Ekaristi Takatifu na Huruma ya Mungu?

Unapofatilia kwa kina na takafari kuu adhimisho la Misa Takatifu utabaini uhusiano uliopo na wenye kujidhirisha wazi kabisa namna Sakramenti ya Ekaristi ni tunu na sehemu ya Huruma ya Mungu kwetu sisi wanadamu.

Kwa ufupi, adhimisho la Ekaristi limejengeka katika kuomba Huruma ya Mungu.

Hebu tuangalie mtiririko mzima wa adhimisho la Misa hasa zile sehemu zenye uhusiano wa moja kwa moja na Huruma ya Mungu;

Sehemu ya kwanza ya Misa: Litrujia ya Neno

Misa huanza daima na ishara ya msalaba ambayo waumini wote kila mmoja lazima waitikie amina. Ni muhimu sana kila muumini kuhakikisha anakuwapo mwanzo misa inaanza kwa ishara ya msalaba na si kukuta misa ipo katikati.

Ishara ya msalaba hii daima hutukumbusha waumini kwamba tumekombolewa kwa msalaba. Ni kwa huruma yake, Kristu alikubali kuuchukua msalaba ili mwanadamu akombolewe.

Muhimu pia tuelewe kwamba, ukombozi ambao unatangazwa kila tufanyapo ishara ya msalaba ni tendo la Utatu Mtakatifu, tendo la umoja wa Mungu na si Yesu Kristu pekee kwani nafsi zote zimeshiriki kikamilifu katika safari ya ukombozi wa mwanadamu. Mungu Baba tumethibitishiwa ushiriki wake pale ambapo aliona wanadamu tumetenda dhambi kisha akahoji nimtume nani (Isaya 6:8); ndipo Yesu Kristu akajibu, nitume mimi Baba. Na hatimaye tunaona ushiriki wa nafsi ya tatu kwa kufanikisha Yesu Kristu kutungwa mimba kwa Mama Bikira Maria (Mathayo 1:18).

Tendo la Toba

Mwanzoni kabisa wa adhimisho la Misa Takatifu, kwa kutambua wanadamu tu wadhambi na ili sala zetu zipate kibali machoni kwa Mungu Padre hualika waumini kutubu;

“Ndugu zangu, tukiri dhambi zetu ili tupate kustahilishwa kuadhimisha mafumbo matakatifu….Namwungamia Mungu mwenyezi…kwani nimekosa mno, kwa mawazo, kwa maneno, kwa vitendo na kwa kutotimiza wajibu…”

Kisha huendelea kuomba huruma ya Mungu wakisali:

“Bwana utuhurumie… Kristu utuhurumie….”

Haifai kuachia kwaya pekee kuimba/kusali sala hii. Ni muhimu sana kwa kila muumini kuisali sala hii hata kama baadhi ya maeneo huisali kwa njia ya nyimbo. Hii pia inapaswa iwe hata katika sehemu zingine za Misa ambazo huimbwa badala ya kutamkwa kama vile sala ya Baba yetu, sala ya Nasadiki (Kukiri Imani) nk.

Kusomwa Injili

Kristu kila leo hugusa nafsi zetu na kuzungumza nasi moja kwa moja kwa kupitia masomo na Injili inayosomwa kila siku katika kila adhimisho la Misa. Si Padre au Msoma Masomo bali ni Mungu mwenyewe ndiye huzungumza nasi na ndiyo maana kila baada ya kumalizika husemwa; “… neno la Mungu”

Kabla ya kusoma Injili, Padre husali akiinamia altare, akiomba huruma ya Mungu, “Ee Mungu mwenyezi, utakase moyo wangu na midomo yangu, niweze kutangaza inavyostahili Injili yako takatifu.”

Baada ya kusoma Injili, Padre hubusu kitabu cha Injili huku akiomba huruma ya Mungu; “Dhambi zetu ziondolewe kwa Injili iliyotangazwa.”

Sehemu ya pili ya Misa : Litrujia ya Ekaristi Takatifu

Sehemu ya pili ya Misa hapa tunashuhudia kiini cha huruma ya Mungu kikijidhihirisha katika adhimisho la Misa Takatifu. Sehemu hii inagawanyika katika vipengele vikuu vitatu (3) yaani; matoleo (maandalizi ya kuifanya Ekaristi Takatifu), mageuzo na kipengele cha mwisho kikiwa ni komunyo.

Matoleo (Offertorio)

Maandalizi ya kuifanya Ekaristi Takatifu huanza kwa vipaji viwili yaani mkate na divai ambavyo ndiyo hutumika kugeuzwa kuwa Mwili na Damu ya Yesu Kristu. Mkate na Divai, ni Yesu anajitoa kushiriki. Na hapa ndiyo moja ya fursa adhimu kwetu sisi waumini kujichotea neema na baraka kutokana na huruma ya Mungu kwani tunapaswa tuguswe na kumtolea Mungu sadaka inayostahili na si mabaki. Kwani, Kristu mwenyewe alijitoa na kukubali kufa msalabani. Tunapaswa pia kujiepusha kutoa kwa kisirani, kwa chuki au manung’uniko kwani yanakosa baraka mbele za Mungu bali tunapaswa kutoa kwa moyo mkunjufu (2 Korintho 9 :7), (1 Petro 4 :9).

Mageuzo

Vipaji vikishakupokelewa altareni, baada ya kuhani kuchanganya divai na maji katika kalisi hali akisali sala za matoleo, kisha Padre huinama sana akiielekea altare huku akiomba huruma ya Mungu; “Tukiwa na moyo wa unyenyekevu na toba tupokewe nawe, ee Bwana, na hivyo sadaka yetu ifanyike leo mbele yako, ili ipate kukupendeza, ee Bwana Mungu.”

Kisha hunawa mikono akisimama pembeni mwa altare huku akiomba huruma ya Mungu; “Ee Bwana unioshe kabisa uovu wangu, unitakase dhambi zangu.”

Hapa pia tunapata fundisho sisi waumini kwamba hata Padre kama binadamu hujinyenyekeza kuomba neema na rehema za Mungu kuweza kufanya adhimisho hili takatifu.

Sala ya Ekaristi

Kiini cha sala ya Ekaristi ni mageuzo. Tunamsikia Padre akisema; “Twaeni mle nyote, huu ndio mwili wangu utakaotolewa kwa ajili yenu….Twaeni mnywe nyote, hiki ndicho kikombe cha damu yangu, damu ya agano jipya na la milele, itakayomwagika kwaajili yenu na kwaajili ya wengi kwa maondoleo ya dhambi….”

Maneno hayo ya mageuzo aliyoyatamka Yesu wakati wa karamu ya mwisho (Yohana 6 :68) ambayo ndiyo msingi wa uwepo wa Ekaristi Takatifu (form of the sacrament) yanadhihirisha wazi kuwa Ekaristi takatifu ni sakramenti ya mapendo ya Kristu kwetu, upendo unaojipambanua katika Huruma yake isiyo kifani….yaani, kuutoa mwili wake, kumwaga damu yake msalabani ili ulimwengu ukombolewe kwa kuondolewa dhambi.

Sala ya Ekaristi-I, baada ya mageuzo, kuhani huendelea kuomba huruma ya Mungu…. “Nasi pia watumishi wako wakosefu, tunaotumainia wingi wa rehema zako, utujalie sehemu ya urithi na ushirika pamoja na mitume na mashahidi wako watakatifu….(hutajwa baadhi ya majina ya mitume na watakatifu… Petro, Felista, Perpetua, Agata, Lusia, Agnesi, Sesilia, Anastasia…)…Tunakuomba, ee Mungu mkarimu, utupokee na sisi katika ushirika wao, si kwa kuhesabu mastahili yetu, bali kwa ajili ya msamaha wako.”

Komunio

Sehemu hii tunaona hatua kwa hatua ya mwanadamu kuomba huruma ya Mungu kwa sala ambazo nyingine husemwa moja kwa moja na waumini wote na nyingine husemwa na Padre kwa niaba ya Kanisa zima.

Huanza na sala ya ‘Baba yetu…’ ambayo hufundisha kwa kina funzo la msamaha, huruma ya Mungu kwetu lakini pia toka kwa Mungu; “…utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea…”

Padre baada ya sala hiyo huendelea kuomba huruma ya Mungu; “Ee bwana tunakuomba utuopoe katika maovu yote… kwa msaada wa huruma yako, tuopolewe daima na dhambi….”

Waamini huitikia na kisha kuhani huendelea kusema; “Ee Bwana Yesu Kristu… usizitazame dhambi zetu ila tu imani ya kanisa lako…”

Kabla Padre hajawaalika kwa komunio, Waamini husema/huomba wakiomba huruma ya Mungu: “Mwanakondoo wa Mungu, uondoaye dhambi za ulimwengu, -utuhurumie…. -utujalie amani.”

Wakati waamini wakiimba/wakisali “Mwanakondoo…”, Padre huendelea kuomba huruma ya Mungu akisema; “Ee Bwana Yesu Kristu, mwana wa Mungu aliye hai, kadiri ya mapenzi ya Baba… uniokoe kwa mwili na kwa damu yako hii takatifu sana, katika maovu yangu yote na mabaya yote; unifanye niambatane daima na amri zako wala usiniruhusu nitengane nawe kamwe.”

Huweza pia kusali sala hii;

“Ee Bwana Yesu Kristu, huku kupokea mwili na damu yako, kusiwe kwangu hukumu na adhabu, bali kwa huruma yako, kunifae mimi kwa kunilinda akili na mwili na kuwa dawa ya kuniponya.”

Padre anapowaalika watu kumpokea Kristu katika maumbo ya mkate na divai husema; “Tazama mwanakondoo wa Mungu, tazama aondoaye dhambi za ulimwengu, heri ya walioalikwa kwenye karamu ya mwanakondoo”

Kwa unyenyekevu waamini huitikia: “Ee Bwana sistahili uingie kwangu, lakini sema neno tu, na roho yangu itapona.”

Baada ya Komunio, kuhani akiwa anasafisha kikombe/Kalisi husali hivi akiomba huruma ya Mungu: “Ee Bwana tulichokipokea kinywani, tukishike kwa moyo safi; na tulichopewa kama zawadi hapa duniani kiwe kwetu dawa ya kutuponya milele.”

Kwa huruma ya Mungu tunaona pia Yesu Kristu alikuwa daima akituhurumia na kutufikiria, kiasi kwamba kwa kutambua kuondoka kwake katika ulimwengu huu

Yesu Kristu daima alikuwa akitufikiria wanadamu, ni kwa neema na huruma ya Mungu tunamuona Kristu akitufikiria na kuona haitafaa kutuacha upweke, ndipo anatuachia “chakula cha uzima” na daima kuhakikisha tunaungana nae kwa kuupokea Mwili na Damu Takatifu. Tunapata bahati hii ya kuweza kuungana nae mpaka hapo ambapo atarudi kwani mwenyewe alishasema; adhimisho hilo lifanywe mpaka atakaporudi.

Hapa tunashuhudia utofauti baina ya Pasaka ya Kristu mfufuka na Pasaka waliyopita Mababu zetu katika Agano la Kale kutoka utumwani Misri (baada ya huruma ya Mungu, akitambua wazi kwamba awali walimuasi na kumkasirisha). Babu zetu katika agano la kale tumeona walikula chakula kile- mana jangwani na baada ya kutoa taabuni na kufika nchi ya ahadi hawakuendelea kupata bahati na neema ya kuimarishwa na chakula cha Mungu.

Komunio Takatifu hututenga na dhambi

Mafundisho ya Kanisa yanatufunulia juu ya namna ambavyo Komunio Takatifu hutusaidia sisi tunaopokea kuweza kuwa katika hali ya usafi. Daima tunasisitizwa kabla ya kupokea, kujitafakari nafsi zetu kama tupo katika hali bora yenye kustahili kumpokea Kristu, na hapo ndipo pia maandalizi kabla ya kupokea sakramenti ya Komunio Takatifu ni muhimu sana kwa kutubu dhambi kupitia kitubio, kupata ondoleo la dhambi na kutimiza malipizi.

Damu ya Kristu iliyomwagika msalabani, kwa ajili yetu kwa maondoleo ya dhambi ni kiini kikuu cha ukombozi wa mwanadamu na kujidhihirisha kwa upendo wa Mungu kwa wanadamu.

“Kwa sababu hiyo, Ekaristi haiwezi kutuunganisha na Kristu bila wakati huo huo kutuosha na dhambi za zamani na kutukinga na dhambi zijazo” (KKK, uk.333)

Kwa kupokea Mwili na Damu Takatifu ya Yesu Kristu, tunaungana na Kristu, tunafia dhambi na kuishi kwa ajili ya Mungu.

Muhimu pia tufahamu kwamba, Ekaristi Takatifu (Mwili na Damu ya Kristu) hutolewa kwa kulipia dhambi zetu wanadamu; walio hai na dhambi hata za walio wafu. Pia huwa kinga kwetu dhidi ya dhambi kubwa.

*Andiko hili ni sehemu ya muswada unaoendelea kuandikwa wa kinachotarajiwa kuwa kitabu juu ya mafundisho ya Kanisa Katoliki kwenye eneo la Huruma ya Mungu

--

--

Michael Dalali

"Truth is an inseparable companion of justice and mercy"-@pontifex| Cogito Ergo Sum| Analyst| Strategist| Facilitator| Translator| Writer & Avid Reader! 🥋