Babu Issa; Ubuyu na tunu za biashara
Kila jambo duniani endapo ukalifanya kwa ufanisi, weledi na ufundi wa hali ya juu hakika utapata utambulisho katika ufanyalo.
Kwa Zanzibar, wapo ambao walikuwa utambulisho na nembo iliyoenda sambamba na kisiwa hicho cha marashi ya karafuu. Bibi Kidude nguli aliyedumu miaka na miaka na kupeperusha bendera vyema ya Zanzibari ni moja tu ya mifano hai.
Hapo ndipo utasikia mtu akijitambulisha natokea Zanzibar; haraka haraka mtu kurukia...oooh kwa Bi. Kidude mwimbaji maarufu...au fukwe nzuri.
Basi bila shaka, jina la Babu Issa nalo limejijengea mizizi na kuwa utambulisho. Yeye upekee wake ni ktk kutengeneza ubuyu wenye ladha ya kipekee. Ndiyo, ubuyu!
Kwa habari nilizopata toka kwa wapenzi wa bidhaa yake ya ubuyu, Babu Issa bidhaa yake hiyo inavuka hata mipaka ya visiwa na bara...ubuyu unafika hata Uarabuni...Ubuyu huo unapanda ndege na kufika mbali kama Marekani na mahala kwingineko. Kulipo Wazanzibari na hata kusiko Wazanzibari. Alimradi mwenye mapenzi au kujaliwa kupata kuuonja ubuyu huo, daima atatamani kuendelea kuula apatapo fursa. Hivyo sitoshangaa ukakuta ubuyu wa Babu Issa hata nchi ambayo hukudhani ungeweza kufika.
Ukiacha utamu na upekee wa ubuyu wa Babu Issa. Kuna funzo kubwa la biashara na uungwana ambao Babu Issa anatufundisha.
Daima Babu Issa anaridhika na bei ambayo anaipa bidhaa yake bila kujali namna gani wachuuzi wengine wanavyoongeza bei katika bidhaa hiyo na kupata faida zaidi.
Mzee huyu anaendelea kutengeneza bidhaa hii pasina kusumbua au kuona kuna wenye kuneemeka kupitia mgongo wake. Anaridhika na kile ambacho ni stahiki yake kadiri ya anavyoona kwa bei yake.
Kwa haraka unaweza ukadhani ni jambo la kawaida na ilipaswa iwe hivi. La hasha! Kuna kundi la watoa huduma au wafanyabiashara wengi ambao huwa hawaridhiki na stahiki zao. Waonapo msururu wa wateja au kufahamu kuna wenye kuneemeka zaidi kupitia huduma na bidhaa zao basi fahamu kuwa wanaweza kufanya mawili; aidha kupandisha bei maradufu kila uchao mpaka ifikie mahala wateja wake washindwe kuhimili.
Au pili, kuanza kukosa uaminifu na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa au huduma yake. Visingizio vinaanza. Kutokutoa huduma au kutengeneza bidhaa ili tu kukata mnyororo wa wale ambao anaamini wanakuwa wanajineemesha kupitia mgongo wake hata kama wamempa malipo stahiki kwa huduma au bidhaa anayozalisha.
Mara nyingi matokeo ya haya huwa ni kuharibu biashara nzima si kwa wale ambao wanakuwa ni wachuuzi rejareja wa bidhaa zake bali hata kwake yeye mwenyewe.
Kwa Babu Issa hii ni tofauti. Na hili ni funzo kubwa sana. Kuhakikisha unaridhika kwa kile ambacho ndicho haki na stahiki yako.
Kwa uwepo wa wauzaji rejareja wa bidhaa yako na wenye kukupatia pato ambalo umelitarajia na kulipanga ndivyo pia ustawi wa biashara na uzalishaji wako. Ni mfumo wa kutegemeana.
Hekima za miaka na miaka ni kwamba; mbio ili mkimbiaji afike mbali, basi akimbie na wenzie lakini mbio zenye kukimbia bila ushirikiano wa wengi huzaa matunda hafifu.
Naamini pia, Babu Issa kazi yake ya ubuyu angalitaka kuikumbatia pekee basi asingaliweza labda kupenya mipaka na mabara. Ila kwa moyo wake wa kutosheka na haki na stahiki anayoipata kunafungua milango bidhaa yake kusambazwa na kufika mahala pengi huku nae akiwa na soko la uhakika.
Kwa wataalamu wa ufungashaji (packaging) kuna hitaji ukiangalia bidhaa za Babu Issa kufanyiwa ufungashaji wa kisasa na kufanya "branding" nzuri. Hii ni fursa hasa kwa kuendeleza utambulisho wa ubuyu wa Babu Issa na hasa endapo tunatamani kuteka soko la dunia.
Babu Issa ni moja ya utambulisho wa Zanzibar. Ni sehemu ya tunu za visiwa vya marashi.