Bikira Maria; kiini cha ukombozi wetu

Michael Dalali
6 min readOct 27, 2022

Safari ya ukombozi wa mwanadamu toka dhambini ina mguso wa kipekee na mafundisho mengi ndani yake. Yesu Kristu, Mungu mwana ambaye alikubali kujishusha na kuuchukua uanadamu, kujisadaka na kutoa uhai wake kwa ajili ya ukombozi wetu ni funzo kuu. Funzo hili si kamilifu pasina uwepo wa Mama yetu Bikira Maria ambaye alikubali kutendewa kadiri ya mpango wa Mungu yaani kwa uwezo wa Mungu Roho Mtakatifu — Kristu ashushwe ndani yake (Luka 1: 26–38)”.

Awali kabisa, tunaona katika kitabu cha Mwanzo 3 : 1–20 mwanadamu alipomkosea Mungu katika bustani ya Edeni ambapo wazee wetu ; Adamu na Eva walipotenda dhambi ya kukosa utii kwa Mungu kwa kutenda kinyume na maagizo yake ; yaani katazo la kutokula tunda la mti wa katikati, mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Tayari ikawa anguko la mwanadamu.

Hapa tunaona funzo kwamba ; ni katika bustani ndipo mwanadamu alianguka. Lakini ni katika Golgotha ndipo alikombolewa. Ni kwa mti ndipo alichuma anguko lake na kupata dhambi ya asili kwa kila mzaliwa wa mwanadamu ; lakini baadae tunakuja kuona ni mti (kwa mfumo wa msalaba) ndipo ukombozi wa mwanadamu unatokea. Na ni kwa mwanamke yaani Eva ndipo anguko la mwanadamu lilianzia na tunaona mwanamke pia anatumika na Mungu kumtoa tena mwanadamu dhambini kwa kukubali kwa Mama Bikira Maria kumzaa Yesu Kristu Mkombozi.

Mama Bikira Maria ndiye kiini cha ukombozi kwa utayari wake kukubali fumbo la ukombozi litokee kwa kuchukua mimba na kumzaa Yesu Kristu. Kwa kukubali kwake (Fiat) ndipo kazi rasmi ya ukombozi wa wanadamu ikaanza.

Swali la msingi na tafakarishi mtu unaweza kujiuliza ni ; Je, ingekuwaje kama Mama Bikira Maria angekataa mwaliko wa Mungu kushiriki ukombozi kwa kuchukua mimba na kumzaa Kristu ?

Swali hili linajibiwa vyema na Fulton Sheen katika andiko lake; “Utangulizi wa dini” (Preface to Religion) kwamba ni kweli Bikira Maria angaliweza kukataa kwani upekee wa binadamu kulinganisha na wanyama wengine Mungu katika uumbaji alitupa utashi. Na ni kwa kutumia utashi huu ndipo tunachagua mema na mabaya. Lakini zaidi, katika machaguo yetu kwa kutumia utashi ndipo sifa, utukufu na ukuu wa Mungu hudhihirishwa zaidi hasa tufanyapo uamuzi mema. Tunapoamua kufanya jema na kuacha baya hata katika maisha yetu tunamtukuza Mungu ; na tunapoacha kuchagua jema na kuamua uamuzi mbaya tunamsononesha Mungu. Hivyo basi, kwa Mama Bikira Maria kukubali kwa utashi wake mwenyewe wito wa Mungu ; utukufu wa Mungu umedhihirishwa.

Lakini Fulton Sheen anakwenda mbali zaidi na kuungana na fundisho muhimu katika imani yetu Katoliki ambalo chimbuko na asili yake lipo katika Biblia — pale Malaika Gabrieli alipomsalimia Mama Bikira Maria ; “Salamu , ewe uliyeneemeshwa na Mungu ! Bwana yuko nawe !….usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema.” (rejea : Luka 1 : 28–30). Bikira Maria hakuwa na dhambi ; kwani alikingiwa dhambi ya asili ili kusudi fumbo la ukombozi litimilizike kupitia yeye. Mungu asingalikaa mahala “pachafu (dhambi)” hivyo alipatakatifuza tangu awali. Na kwa mantiki (logic) hiyo, Mama huyu kwa neema na kuwa na Mungu ndani yake asingalienda kinyume na Mungu kwani Mungu alikuwa naye.

Kumbe basi nasi tunaalikwa kumruhusu na kuhakikisha Mungu anakuwa nasi (kwa kujitakatifuza kupitia maungamo na kuishi mwenendo bora), Mungu anakuwa ndani yetu tutapata neema ya kipekee na kudumu katika usafi na kuwa kioo cha Mungu (reflection of God).

Muhimu pia kuzingatia, Mama Bikira Maria hakushurutishwa au kulazimishwa. Bali Mungu alimpa mwaliko. Hapa tunaona ; Mungu daima hutupatia mialiko mbalimbali ya uwokovu katika maisha yetu pasina shuruti na ni hiari yetu kukubali kuenenda kadiri ya mwito wake au kukataa na kubaki katika njia zetu.

Ni rahisi katika mafundisho kutokubaini ugumu na hatari ambayo Mama yetu huyu, Bikira Maria alikuwa nao wakati anapashwa habari na Malaika Gabrieli kwamba atapata ujauzito na kumzaa mkombozi (Luka 1 : 26–38). Na si ugumu tu bali hata alighubikwa na hofu. Na ndiyo maana hata Malaika Gabrieli alimtoa hofu ; “usiogope Maria”.

Kwanza kabisa, Mama Bikira Maria alikuwa ameposwa na Yosefu ; hivyo yupo katika kipindi cha mpito kuelekea ndoa. Ni ngumu katika mazingira hayo si tu kumwambia mchumba wake (Yosefu) bali hata ndugu zake na jamii yote iliyomzunguka habari kwamba ana ujauzito tena ujauzito huo sio wa Mume mtarajiwa (Yosefu) na zaidi hakuwa na uwezo wa kumtaja au kumuonyesha Baba mhusika wa ujauzito huo maana unasema ulitokewa na Malaika na kuambiwa utaupata kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Tafakari tu hata katika mazingira ya leo sakata hili lingekuwa na sura gani ? Angeeleweka kweli Bi Kharusi mtarajiwa kwa maelezo na hali yake ?

Tufahamu, jamii ya kwao na kipindi hicho sheria zilikuwa kali zaidi. Hali ile ya kupata ujauzito katika mazingira yale yangaliweza kabisa kupelekea katika adhabu ya kupigwa mawe mpaka kufa. Hii ina maana, Bikira Maria alikuwa tayari kufa kwa ajili ya kuhakikisha safari ya ukombozi inatimia. Aliweka maisha yake rehani.

Lakini hapa Mama huyu mstaajabivu, alishiriki agano la ukombozi baina ya Mungu kwa wanadamu. Akakubali Mungu mwana, Yesu Kristu akae tumboni mwake. Mama Bikira Maria akawa sanduku la agano kama ilivyokuwa sanduku la agano katika agano la kale baina ya wana wa Israeli na Mungu. Mama Bikira Maria ndiye sanduku jipya la agano kwetu.

Hapa pia, tunapashwa kupata funzo toka kwa Mtakatifu Yosefu, Baba Mlishi wa Yesu Kristu. Anatuonyesha unyenyekevu, usikivu, utulivu, hekima na busara. Kwani hata katikati ya kuwa katika hali isiyokuwa na majibu yenye kutosheleza na kueleweka kibinadamu, anakuwa mtii kwa mwito wa Mungu kumchukua Mama Bikira Maria. Anakuwa tayari kubeba msalaba. Anakuwa tayari kuendeleza uchumba ambao kwa jicho la kibinadamu ni rahisi kusema uchumba ulioingia dosari ya ujauzito ambao sio wa kwake na mwenye ujauzito hamfahamu.

Tukiangalia hata kuja kwake duniani Bwana wetu Yesu Kristu, ukiachia sintofahamu na taharuki hiyo ya kutungwa mimba kwa uwezo wa Mungu Roho Mtakatifu na kuchukua mwili. Hata lile tendo lenyewe la kuzaliwa linatafakarisha.

Mpaka sasa, serikali na jamii kwa ujumla inajitahidi kuhakikisha uzazi unakuwa salama hii ni sambamba na kuhakikisha mahala pa kujifungua panakuwa na mazingira bora, uwepo wa wataalamu — madaktari na wakunga. Lakini haikuwa hivi kwa wakati wa kuzaliwa kwa Yesu Kristu kwani Mama Bikira Maria alipitia wakati mgumu baada ya kukosekana pahala ka kufikia iliwapasa wajibanze katika zizi la ng’ombe. Na huko ndiko alipojifungua.

Lazima mazingira hayakuwa rafiki ; hivyo aliweka maisha yake rehani kwa kuhatarisha usalama wake (Mama) na mtoto. Hii yote ni katika kutimiliza fumbo la ukombozi wa mwanadamu.

Mama Bikira Maria kuwa kwake kiini katika safari ya ukombozi hakukomi kwa Kristo Yesu kufa msalabani pale Golgotha. Kunaendelea mpaka leo na hata kesho — daima na milele.

Yeye anaendelea kuwa kiunganishi kati ya Mungu na wanadamu katika kuhakikisha hakuna mwanadamu yoyote anapotea. Yeye anaendelea kuwaombea wakosefu waongoke.

Tunakumbuka habari ya tokeo la Mama Bikira Maria huko Fatima 1917 kwa watoto Lucia, Fransisko na Yasinta. Msisitizo mkubwa wa ujumbe wake Mama yetu Bikira Maria ulikuwa ni kuwaombea wakosefu ili waongoke. Hii inadhihirisha kwamba hajatusahau na hata awapo mbinguni bado anaumia pale mwanadamu anapoanguka dhambini. Hapendi mwanadamu yoyote apotee. Anaendelea na kazi ya ukombozi hata leo.

Nasi wanadamu, kila uchao tunakumbushwa huyu ndiye mwombezi wetu kwa mwanae Yesu Kristu. Tunaalikwa tumkimbilie yeye nyakati zote. Tunaalika tufanye sala zetu na maombezi yetu kupitia kwake kwani sauti yake ina namna ya kupenya kwa Mungu mwana, Yesu Kristu na kupokelewa kwa huruma na utii wa mwana kwa mama. Mama Bikira Maria anaendelea kubaki kuwa kiini cha ukombozi hata sasa. Kama ilivyo sifa yake kati ya nyingi katika litania ya Bikira Maria; yeye ni “mlango wa mbingu”. Ni kwa kupitia yeye na maombezi yake tunaiona mbingu. Basi karibuni bila kuchoka kuhakikisha kufanya sala na maombezi kwa Mama yetu Bikira Maria.

Ave Maria!

--

--

Michael Dalali

"Truth is an inseparable companion of justice and mercy"-@pontifex| Cogito Ergo Sum| Analyst| Strategist| Facilitator| Translator| Writer & Avid Reader! 🥋