Chaguzi huru na haki ni upi?

Michael Dalali
9 min readMay 20, 2022

Tunaweza kujihoji, je tunaweza kweli tukawa na uchaguzi unaoaminika, huru na wa haki? Na je, nini kifanyike ili chaguzi zetu ziwe zinazoaminika, huru na zisimamie haki ? Na hata tunaweza jihoji, sifa na vigezo gani vinatumika kupima chaguzi zinazoaminika, wa huru na haki ?

Wasomi wa taaluma ya sayansi ya siasa wanasema kuna vigezo (nguzo) ambazo ni muhimu sana katika kupima chaguzi ili kuweza kutoa tathmini juu ya chaguzi kuwa huru na haki. Sehemu ya nguzo hizo muhimu ni pamoja na uwazi, usawa, fursa sawa ya kushiriki, uwajibikaji, uadilifu, na haki.

Tukiangalia safari ya chaguzi kuu nchini kwetu kuanzia pale Tanzania tuliporejesha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na kisha kufuatiwa na uchaguzi wa mwaka 1995 na chaguzi zilizofuata, kuna funzo kubwa katika kila chaguzi.

Zipo hatua njema ambazo nchi imewahi kupiga katika kila chaguzi na kwa upekee wake. Lakini pia tunapashwa kuzitambua changamoto na kasoro ambazo zimekuwa zikijitokeza katika chaguzi ama pia kujirudia mara kwa mara.

Shukrani: Katuni na Kingo

Pia tunapashwa kutambua uwepo wa maafisa wasimamizi wa chaguzi ambao licha ya msukumo mbalimbali walimudu kuwa imara na kusimamia maadili ya usimamizi wa chaguzi na kusimamia haki. Wapo ambao kwa misimamo yao ya kusimamia haki na usawa katika chaguzi imegharimu ajira zao au ustawi wao kwa ujumla. Tunatambua sadaka zao kuu kwa ujenzi wa demokrasia imara katika nchi yetu. Majina yao yatadumu katika upande wa wema wa historia yetu na kuandikwa kwa wino wa dhahabu.

Lakini pia wapo maafisa wasimamizi wa chaguzi ambao hawakuwa imara na kukubali kuyumbishwa na msukumo mbalimbali na kuwafanya kupoka haki za chaguzi, walihusika kutia doa na kuleta dosari. Hawa kwa matendo yao ; tutaendelea kuwa funzo muhimu la kuepuka kwa siku za usoni kusudi yasijirudie tena.

Kwa miaka nenda rudi, Tume ya uchaguzi, imekuwa ililalamikiwa sana hasa na vyama vya upinzani katika namna ya usimamizi na uratibu wa chaguzi. Malalamiko yamekuwepo hata nyakati ambazo vyama vya upinzani vimeweza kupata viti vingi katika nafasi za udiwani na ubunge.

Ukiangalia kwa kina, sehemu kubwa ya malalamiko chimbuko lake hasa ni pale ambapo nguzo zile za kidemokrasia za kupima chaguzi kama ni ya huru na haki kwa namna moja au nyingine unakuta zimekiukwa au kutokutendwa kwa kiasi cha kuridhisha pande zote za ushindani.

Je, kwa kuwa na Tume huru ya uchaguzi itakuwa mwisho wa yote haya ?

Tunashawishika kuona kuwa na Tume huru pekee si suluhu ya kudumu ya kasoro na changamoto katika chaguzi zetu hasa bila utashi na dhamira ya dhati ya kuhakikisha uwepo wa usawa na haki katika chaguzi sambamba na kukubali kushindwa katika ushindani na kukabidhi kiti iwe katika ngazi yoyote ya kiuongozi.

Tunatambua mzunguko wa uchaguzi (election cycle) ni gurudumu endelevu, na ndiyo maana hata kuna usemi wa mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa uchaguzi mwingine. Na katika gurudumu hilo endelevu la matukio kuelekea uchaguzi yote huwa na athari kubwa katika kuwa na uchaguzi huru na wa haki.

Pia yapo maswali ya msingi sana ; Je Tume huru maana yake ni nini ? inapatikana vipi ? na Je, mwisho wa siku si lazima awepo mtu mmoja wa kuteua ? Majibu ya maswali haya yanapatikana katika Rasimu ya Warioba, Sehemu ya Pili, Tume Huru ya Uchaguzi kuanzia Ukurasa wa 73–77. Rasimu hii ya Warioba imetusaidia sana kutupa mfano mmojawapo wa kuweza kupata Tume huru ya Uchaguzi. Rasimu ya Warioba kwa ufupi ilipendekeza yafuatayo :

Kwanza kabisa inaeleza umuhimu wa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi. Rasimu hiyo inaeleza muundo wa Tume, majukumu ya Tume, namna ya kushughulikia malalamiko, sifa za Mwenyekiti, Makamu na Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi. Muhimu zaidi Rasimu ya Warioba inapendekeza uwepo wa Kamati ya Uteuzi. Wajumbe wa Kamati hii wanapendekezwa kuwa ni Jaji Mkuu ambaye atakuwa Mwenyekiti, Spika wa Bunge ambaye atakuwa Makamu Mwenyekiti, Spika wa Bunge la Tanganyika, Jaji Mkuu wa Tanganyika, Jaji MKuu wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Tume ya Maadili Uongozi na Uwajibikaji, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi atakuwa Katibu wa Kamati ya Uteuzi.

Kamati ya Uteuzi itakuwa na jukumu la kupokea na kuchambua majina ya watu waliomba na waliopendekezwa kuwa katika Tume Huru ya Uchaguzi kwa mujibu wa utaratibu utakaowekwa na sheria. Rais atateua Mwenyekiti, Makamu na Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi kutoka miongoni mwa majina yaliwayowasilishwa na Kamati ya Uteuzi na Rais atawasilisha majina hayo Bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa na Bunge.

Aidha Rasimu inapendekeza kuwa asasi za kiraia na zisizo za kiserikali zinaweza kupendekeza majina ya watu wanaoweza kuteuliwa kuwa Mwenyekiti, Makamu na Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi. Pia Rasimu ilitoa pendekezo zuri kuwa Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi atateuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Umma. Vivyo hivyo, Msajili wa vyama vya siasa naye atateuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Umma.

Mapendekezo haya mazuri ni katika jitihada za kuweka uwanja sawia, kuondoa malalamiko na kuwa na mchakato ambao ambao angalau kwa kiasi fulani utaweza kutupa Tume Huru ya Uchaguzi na inayokubalika na wadau wote. Tujiulize je kuna dosari gani katika mapendekezo haya ? Ni kipi hakifai ? na kwa nini ? Kamati ya Warioba ilijaribu kufanya uundaji wa chombo hiki uwe ni mchakato na usiwekwe mikononi mwa mtu mmoja kuamua. Kama tulivyoona vyombo mbalimbali vinashiriki ikiwa ni pamoja na Bunge ambalo ni chombo cha uwakilishi cha wananchi.

Je tutafikiaje kuwa na chaguzi huru na wa haki?

Hebu tuangalie kwa uchache baadhi ya vigezo muhimu ambavyo vikizingatiwa vinaondoa shaka kwa wananchi na kuhakikisha imani, haki na uhuru wa uchaguzi unakuwapo kwa kiwango cha juu.

Uwazi katika mchakato mzima wa uchaguzi ; zoezi na kila hatua ya uchaguzi inapashwa iwe ya wazi hasa kwa wananchi na wadau wa karibu wa zoezi zima la uchaguzi mathalani vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki katika zoezi la uchaguzi. Uwazi huu unaanzia katika kupangwa ratiba na siku muhimu za uchaguzi yaani kutangazwa kwa uchaguzi, tarehe ya kupiga kura, kuanza kwa utoaji wa fomu kwa wagombea, ratiba ya urejeshwaji wa fomu, kampeni nk. Katika dunia ya sasa ya matumizi ya mifumo ya kieletroniki katika ukusanyaji matokeo ; ni vyema pia wadau muhimu na wa karibu wa chaguzi kupewa fursa kuhakiki na kujiridhisha juu ya mifumo ya kieletroniki ambayo itatumika ili kuondoa shaka na malalamiko ya mianya ya “uchakachuaji”.

Fursa sawa ya ushiriki ; hii ni eneo pana sana hasa katika chaguzi. Wananchi na wagombea kutoka katika vyama mbalimbali wanapashwa wapewe fursa sawa ya kushiriki mchakato mzima wa zoezi la chaguzi. Hakupashwi kuwe na mazingira yoyote ambayo yanatoa fursa zaidi kwa mshindani mmoja katika zoezi la uchaguzi. Katika chaguzi zetu, tumekwisha kushuhudia mizengwe na ubinyaji wa fursa sawa ya ushiriki kwa raia na hata vyama husika vya kisiasa mathalani kutokuheshimiwa kwa ratiba za kampeni au kuzuia wagombea au vyama fulani kufanya kampeni katika baadhi ya maeneo au ambapo wanaruhusiwa kufanya kampeni basi kumekuwepo nyakati zingine bughudha na kuingiliwa na vyombo vya usalama (hata kama hawajavunja sheria, taratibu na kanuni za usalama au chaguzi). Lakini hizi kwa upande wa vyama shindani wamekuwa wakiona ni mbinu chafu zinazotumiwa kuwarudisha nyuma katika ushindani. Hapa dawa ni kutoa uhuru (wenye kuheshimu sheria, kanuni na taratibu) kwa wote kutenda kwa usawa na amani shughuli zao za kisiasa na kampeni.

Kwa fundisho la uchaguzi mkuu 2020 pia, tunaona fursa sawa ya kushiriki na ushindani pia inaweza kuondoshwa pale ambapo tunakuwa na wagombea wengi wanaopita bila kupingwa. Hapa kutokuingia katika kampeni, kunadi sera, kuwapa fursa wananchi kuchagua kwa kigezo cha mgombea amepita bila kupingwa si sahihi na kitia doa zoezi la uchaguzi kwa mapana yake hasa endapo sababu za kuengua washindani wengine wote zinakuwa hazina mashiko sana. Mantiki pia inakataa hasa kwamba miaka nenda rudi ambao wanapita bila kupingwa huwa wanatokea chama tawala pekee ; ina maana hakuna nyakati kumekuwa na makosa hata madogo kwa wagombea wa chama tawala kuwafanya waenguliwe ila ni kwa wagombea wa vyama shindani tu ?

Uwajibikaji ; kwa watendaji na wasimamizi wa chaguzi wanapashwa watambue wajibu wao. Wanapashwa watambue kwamba matendo yao yanauwezo mkubwa wa kujenga demokrasia yetu au kuibomoa. Wanapashwa daima wasimamie haki, sheria na taratibu bila kushiriki au kuwezesha chama au mgombea mmoja kupata upendeleo dhidi ya wengine kwa hujuma. Labda tuangalie mifano hai michache ; kumekuwa na maafisa chaguzi ambao wanapashwa wawepo na kutoa fomu kwa wagombea toka vyama vyote lakini kwa baadhi ya maeneo tumeshuhudia maafisa hawa wakishiriki hujuma kwa kuhakikisha mgombea wa chama wanachokikusudia akishachukua fomu wao “wanaingia mitini” na kuacha adha kubwa kwa wagombea wengine.

Tufahamu, eneo hili la chaguzi ni moja ya eneo kongwe kupata kuwa katika dunia na kumekuwepo na tafiti na maandiko mbalimbali yenye kujaribu kuangazia eneo hilo toka enzi za Cicero miaka ya 64BC ambapo aliandika kitabu chake cha “How to win an election” (Namna ya kushinda chaguzi) hadi hivi karibuni kwa wanazuoni na wanataaluma wa sasa kama Nic Cheeseman na Brian Klaas na kitabu chao; “How to rig an election ”(Namna ya kuiba uchaguzi).

Shukrani: Katuni na Kingo

Hapa tunaona namna mikakati ilivyoanikwa ya namna gani kwa kusudi kuhakikisha chaguzi zinakuwa si za huru na haki na kwa upana zaidi kuhakikisha chama kilichopo madarakani kinaendelea kulinda nafasi zake dhidi ya washindani wake. Mengi yaliyobainishwa na pia mengine mapya kwa maana mbinu na mikakati mingi imekuwa ikijidhihirisha katika chaguzi nyingi hasa nchi za Afrika (na Tanzania ikiwemo).

Mwanazuoni Nic Cheeseman na mwenzake Brian Klaas katika kitabu chao “namna ya kuiba uchaguzi” (How to rig an election) ukurasa wa 31 wanasema; “mbinu yenye werevu ya kuiba katika uchaguzi ni mapema kabisa kabla ya hata kura hazijachapwa…. kwa dunia ya leo, watawala huiba kabla ya siku ya kupiga kura” (The smartest way to rig an election is to do so before the ballors have even been printed……Today, the most effective autocrats steal elections well before polling day).

Tumeshuhudia mizengwe mingi ikianza toka katika zoezi la kuandikisha wapiga kura, kutambua mipaka ya maeneo ya kiuchaguzi, na ugawaji wa majimbo wa kimkakati. Mbinu zingine ambazo zinazidhirisha pia ukosefu wa dhamira ya dhati ya kuheshimu zoezi la uchaguzi na kuhakikisha haki na usawa unatendeka ni pamoja na ucheleweshaji wa makusudi wa vifaa vya uchaguzi, kutokuonekana kwa majina ya baadhi ya wapigakura katika daftari la kudumu katika eneo husika, kutokubandikwa kwa majina ya baadhi ya wapigakura katika baadhi ya maeneo kama moja ya mbinu chafu ya kudhoofisha wagombea ambao wanakubalika zaidi kuliko washindani wengine.

Hizi ni mbinu chafu ambazo lazima zikemewe daima kwani ni chachu ya machafuko na kuleta madhara mengine ambayo yangeweza kabisa kuepukika.

Kama nchi tumeshashuhudia madhara ya matendo kama hayo kupelekea hata umauti wa watu wasio na hatia, tukijikumbusha namna kifo cha binti Akwilina Akwilini kilivyotokea baada ya wagombea wa CHADEMA kufanyiwa mizengwe katika zoezi la fomu kisha wakaamua kuandamana kupinga kitendo kile ambapo polisi wakatumia risasi za moto kuwatawanya waandamanaji na risasi moja ikampata maheremu Akwilina.

Katika zama za teknolojia ya mtandao, tumeona pia mbinu chafu zingine za kufanya hujuma katika chaguzi zikiendeshwa kwa kutumia mitandao. Hivyo zoezi zima kuanzia kutangazwa kwa uwepo wa uchaguzi, kampeni, uchukuaji wa fomu, upigaji kura nk hadi kuingiza taarifa katika mifumo ya kimtandao kunaweza kusimamiwa na kufanywa vyema kabisa. Kisha inapokuja katika kuingiza taarifa na namna taarifa zinafika katika mahala pa kufanyia majumuisho ndipo mfumo unachezewa kutoa taarifa tofauti na za awali zilizoingizwa.

Inasemekana kutokana na uzoefu wa baadhi ya nchi, mitandao imeweza kuingiliwa au kuhujumiwa na kuja na matokeo tofauti na uhalisia katika karatasi halisi endapo wakihesabu moja moja. Hii imekumba hata nchi zilizoendelea na zenye kuangaliwa kama kioo na za kuigwa mfano kama Marekani.

Baadhi ya kasoro za kimkakati za chaguzi zinavyofanywa mapema kabisa kabla hata “joto” la uchaguzi kuanza kupanda zinakuwa ngumu hata kwa waangalizi wa uchaguzi mbalimbali kuzibaini kwani zinafanywa kwa ustadi wa hali ya juu.

Ni muhimu sana kuwa na dhamira safi na dhati ya kutaka kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki. Unaanzia kwa utashi na dhamira ya viongozi ambao wapo madarakani kwa wakati huo. Ni muhimu sana kuishi kile ambacho daima tumehubiriwa na Mwalimu Julius Nyerere kwamba ili tuendelee tunahitaji pamoja na mengine uwepo wa siasa safi! Ni kwa uwepo wa viongozi wenye weledi, upeo, hofu ya Mungu na wasafi ambapo wanaweza kuhakikisha uwepo wa mifumo, sera, sheria na taasisi imara na huru ambayo itasimamia na kuhakikisha haki na usawa daima vinapatikana.

Tudhamirie kupiga hatua katika eneo hili, tudhamirie kusimamia siasa safi kwa ustawi na maendeleo ya taifa letu. Tukubali kuweka mifumo, sheria, taratibu na hata kanuni ambazo zitachangia kujenga kwa mapana usawa, haki na demokrasia.

Na Michael Dalali na Selemani Rehani

--

--

Michael Dalali

"Truth is an inseparable companion of justice and mercy"-@pontifex| Cogito Ergo Sum| Analyst| Strategist| Facilitator| Translator| Writer & Avid Reader! 🥋