Chaguzi zinazoaminika, huru na haki: dhana yenye changamoto nyingi

Michael Dalali
9 min readMay 18, 2022

Kumekuwa na mjadala muhimu sana wa kisiasa wa kuangalia chaguzi zetu na zaidi unaenda mbali kutafuta “muarubaini” wa kuhakikisha chaguzi zinakuwa zinazoaminika na pia huru na za haki. Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan alipokuwa akipokea ripoti ya “Kamati ya Mukandala” nae aligusia juu ya hoja ya Tume huru na kwenda mbali kuhoji endapo ndiyo hatua tatuzi kwa changamoto za chaguzi.

Kwa taifa kuwa na mjadala mpana wa kujitafakari na kuangalia mwenendo wa chaguzi zetu na kufikiri ni namna gani tunaweza kuziboresha kuhakikisha zinakuwa zenye kuaminika, huru na haki ni jambo la tija na afya sana. Tafakari hii inapashwa iwe huru na isisukumwe na ubinafsi wowote iwe wa kulinda nyadhifa na madaraka au kujipendekeza kwa watawala. Tufikiri na kutafakari kwa kuangalia mustakabali wa leo na kesho ya taifa letu.

Ni maoni yetu kuwa iwapo tunataka kuwa na chaguzi zinazoaminika, huru na za haki ni lazima tuanze kwa kuwa na mfumo mzuri wa kisheria unaotupa uwanja sawia wa ushindani wa kisiasa. Tuanze kwa kuwa na sheria mama au katiba bora inayokubalika na wadau kutoka katika asasi mbalimbali za kiraia, vyama vya siasa ikiwa ni pamoja na vyama vya upinzani, wananchi kwa ujumla na wadau kutoka makundi maalum. Hatuwezi kuwa na chaguzi zinazoaminika iwapo kama ilivyo sasa, tuna katiba ambayo inakubalika na watawala tu au chama kilichopo madarakani.

Sheria mama bora ni muhimu sana, kwani sheria nyingine zote zitatokana na katiba ikiwa ni pamoja na sheria zote zinazohusika katika kusimamia uchaguzi. Ni vyema hapa tukataja mapungufu machache tu yaliyopo katika sheria mama yetu/katiba ambayo kwayo yanawanyima Watanzania kuweza kuwa na uchaguzi unaoaminika, huru na wa haki.

Katiba yetu ya sasa inawanyima haki yao ya uraia kwa Watanzania ambao si wanachama wa chama chochote cha kisiasa kuomba kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi kama vile udiwani, ubunge na Urais. Ibara 5, 39 (b) na 67 (b) zinabainisha na kuweka sharti lazima raia awe na chama ndipo apate fursa ya kugombea. Hebu tuangalie mfano wa Ibara ya 67 (b) inasema sifa ya mtu kugombea nyadhifa ya ubunge ni lazima awe ; “mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa”.

Watanzania hatuna budi kuwauliza watawala, iwapo katiba yetu inatambua uhuru wa kujumuika na kujiunga na chama chochote, kwa nini tunyimwe haki yetu ya kuomba kuchaguliwa? Kutojiunga na chama chochote pia ni haki ya Watanzania. Kwa nini tulazimishwe kujiunga na vyama vya siasa ili tuweze kuomba kura kwa Watanzania wenzetu? Hii ni haki yetu ya uraia, ni nani mwenye mamlaka ya kupoka haki ya uraia? Hatuwezi kuwa na uchaguzi huru na wa haki iwapo mamilioni ya Watanzania ambao kwa sababu zao za msingi si wananchama wa chama chochote kile, wanaendelea kunyimwa haki yao ya uraia ya kuomba kuchaguliwa bila kujiunga na chama chochote cha siasa.

Katiba yetu tuliyonayo, hairuhusu mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili mikuu mitatu yaani Bunge, Serikali (Dola) na Mahakama. Katiba yetu ya sasa inayolindwa na watawala kwa gharama kubwa inatoa nguvu kubwa sana kwa mhimili mmoja wa Dola na kuifunika mihimili mingine. Aidha inampa madaraka makubwa sana Rais ambaye kwa utamaduni uliopo huwa ndio anakuwa Mwenyekiti wa chama tawala. Madaraka hayo makubwa ni kuteua wakuu wa taasisi zote, mawaziri, manaibu waziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, mabalozi, Wakuu wa Vyombo na Taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Taasisi zinazosimamia uchaguzi (Electoral management bodies). Vyombo hivi ni pamoja na Tume ya Uchaguzi, na Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.

Ibara ya 36 (2) inasema ; “Rais atakuwa na madaraka ya kuteua watu wa kushika nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za idara na taasisi za Serikali, na watendaji wakuu wanaowajibika kusimamia utekelezaji wa sera za idara na taasisi hizo katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, nafasi ambazo zimetajwa katika Katiba hii au katika sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge kwamba zitajazwa kwa uteuzi unaofanywa na Rais.”

Tukumbuke, Rais ambaye mara nyingi huwa ni Mwenyekiti wa chama chake mathalani kwa sasa, Rais ni zao la Chama cha Mapinduzi na ni Mwenyekiti wa chama hicho anamteua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi; Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi; Makamishna wote wa Tume ya Uchaguzi, Msajili wa vyama vya siasa, Wakurugenzi ambayo pia huwa maofisa wa kusimamia uchaguzi (returning officers).

Shukrani: Katuni na Masoud Kipanya

Hivyo ili tuwe na uchaguzi wa kuaminika, huru na wa haki hatuna budi tuwe na Katiba ambayo inatupa watanzania mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili mitatu, pia Katiba ambayo itatupa vyombo huru vinavyosimamia uchaguzi, vyenye uwezo, na visivyoegemea upande wowote. Kwa Katiba ya sasa hatuna tume huru, inayokubalika na inayoaminika na wadau wote. Tume tuliyonayo sasa inakubalika zaidi na watawala, na sababu za wao kuikubali zipo wazi.

Rais wa kwanza kuchaguliwa katika siasa za demokrasia ya mfumo wa vyama vingi, Marehemu Benjamin Mkapa aliandika katika kitabu chake cha ‘My Life, My Purpose’ (Maisha Yangu, Kusudi Langu) kuwa muundo wa tume umekuwa miongoni mwa masuala yanayopigiwa kelele na kupata upinzania mkubwa kutokana na upatikanaji wa viongozi wake. Anasema kuwa ‘kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi inayokubalika na vyama vyote vya siasa ndio chachu ya kulea na kukuza demokrasia nchini’. Mkapa alitahadharisha kuwa muundo wa tume umekuwa miongoni mwa masuala yanayopigiwa kele na kupata upinzania mkubwa kutokana na upatikanji wa viongozi wake.

Kukosekana kwa mgawanyo wa madaraka kunapelekea hata vyombo vingine kama vyombo vya usalama, jeshi la polisi, vyombo vya habari n.k kushindwa kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa huru na wa haki na hawaegemei upande wowote.

Tunakumbuka katika uchaguzi mkuu uliopita (mwaka 2020) tulishuhudia kusambaa kwa “picha za video zilizokuwa zikumuonyesha afisa wa polisi wa cheo cha juu (OCD), Kamanda Mpina akiwa katika sare za kazi na katika muda wa kazi akiingilia shughuli za kisiasa na kuzuia huku akimwambia kiongozi mkuu wa chama kimoja cha upinzani, Freeman Mbowe (ambaye alikuwa ndani ya jimbo lake Hai kama mgombea katika shughuli za kampeni) kuwa safari hii kwa namna yoyote hatoshinda. Jambo lile ni hatari kisiasa na hasa kwenye jamii inayoamini demokrasia kwani msimamizi wa usalama ambaye haruhusiwi kudhihirisha hadharani hisia au msimamo wake binafsi wa kisiasa alithubutu kufanya hivyo jambo ambalo linatia doa dhana nzima ya usawa na haki katika chaguzi.

Katiba ya sasa inawanyima nafasi na uhuru wa kuhoji matokeo ya Urais. Katiba ibara ya 41 (7) inasema ; “Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake. Ni wakati muafaka kwa Watawala kuwaeleza Watanzania kuna mantiki gani ya kuwanyima Watanzania fursa ya kuhoji matokea ya Urais? Kama matokeo ya ubunge na Udiwani yanahojiwa, iweje matokeo ya Urais yasipingwe na kuhojiwa katika vyombo vya utoaji wa haki!

Katiba iliyopo pia inatoa nafasi kubwa sana kwa mgombea ambaye anatetea nafasi yake kushinda kwa mara nyingine (Incumbancy advatange). Mara nyingi tumeona mgombea aliyopa madarakani akitumia nafasi yake (tunaweza kusema vibaya) kutoa vitisho, kutoa ahadi, maagizo na amri ya kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili wapiga kura wakati wa kampeni. Tunakumbuka matamshi mazito ya Katibu Mkuu wa CCM wakati wa Uchaguzi Mkuu 2020, Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ambapo alisema atahakikisha anatumia dola kushika dola; chama chochote kilichopo madarakani kikashindwa kutumia dola na madaraka yake kubaki katika dola basi ni uzembe wake wenyewe !

Shukrani: Katuni na Masoud Kipanya

Mifano mingine, Raisi ambaye kwa wakati huo huo ni mgombea akitumia vibaya nafasi yake na kukiuka kanuni za chaguzi huku wasimamizi wa chaguzi wakafumbia macho ni kuanza kutishia wasimamizi wa uchaguzi, imepata tokea wasimamizi wanaambiwa nimekupa gari, nyumba na nakulipa mshahara kisha unamtangaza mpinzani au kufika mahala akiwa katikati ya kampeni anakuta tatizo anampigia Waziri au Katibu Mkuu na kumpa agizo jambo hilo litatuliwe mara moja. Ni wazi kuwa uchaguzi kama huo hauwezi kuwa huru na wa haki.

Pia tumeona wagombea ambao wapo madarakani wakitumia rasilimali za serikali katika kampeni. Vitendo hivi vyote hutia najisi chaguzi zetu. Katika ripoti yao ya uangalizi wa uchaguzi 2020, Taasisi maarufu hapa nchini ijulikanayo kama ‘Research and Education for Democracy in Tanzania (REDET) au Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania, inayoongozwa na Mwenyekiti na Mbobezi wa Sayansi ya Siasa, Profesa Rwekaza S. Mukandala ambaye pia kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kikosi Kazi kilichoundwa na Mh. Rais ili kukusanya maoni ya wadau katika kuboresha mazingira ya kisiasa nchini, imebainisha mapungufu kadhaa katika uchaguzi wa 2020 ambayo ni vyema tukayarekebisha.

Baadhi tu ya mapungufu yaliyobainishwa na REDET ni pamoja na mgombea kupitia CCM kutoa ahadi na kufanya maamuzi kama Rais na hivyo kushindwa kutofautisha kati ya Rais na mgombea. Tarehe 13 September 2020, wakati wa ziara ya kitaifa, Rais Museven wa Uganda alimuunga mkono mgombea wa CCM na kusema anamuombea Mungu ashinde, wakati akifanya kampeni katika jimbo la Ubungo, mgombea wa CCM alitoa agizo kuwa soko la Mahakam aya Ndizi liwe chini ya wananchi na sio kiwanda cha Urafiki ; pia alitoa amri ya kusimamisha ulipaji wa kodi kwa wafanyabiashara wadogo wadogo. Mwenendo huu ulikuwepo pia kwa wagombea wa Ubungo ambao pia ni mawaziri, kwa mfano, Waziri Suleimani Jasso alipokea msaada wa vifaa vya ujenzi wenye tthamani ya milioni 17 kutoka kwa Benki ya National Micro-Finance (NMB) kwa ajili ya ujenzi wa shule katika jimbo la Kisarawe ambalo yeye alikuwa ni mgombea.

Pia ripoti hii inaeleza matumizi ya viongzi wa dini katika kampeni ambapo inaeleza vyama vyote vikubwa viliwatumia viongozi wa dini wa dini katika kufanya kampeni. Kwa maoni yetu hii ni hatari ambayo inaweza kuingiza nchi katika migongano ya kidini. Ripoti ya REDET, pia inaeleza kuwa zoezi la uangalizi wa uchaguzi liliathirika kutokana na uamuzi wa serikali kuleta sheria ambayo ilipiga marufuku asas za kidini kushiriki katika kutoa elimu ya upigaji kura na uoangalizi wa chaguzi. Ni jambo la kutia moyo kuwa Mwenyekiti wa Kikosi Kazi pia ndio Mwenyekiti wa REDET, hivyo kuna nafasi adhimu ya kusahihisha yale ambayo yamebainishwa katika ripoti ya REDET.

Ili tuweze kuwa na chaguzi zinazoaminika, huru na za haki, ni lazima pia tuangalie sheria zetu mbalimbali ambazo zina athari za ama moja kwa moja au kugusa chaguzi zetu. Kuanzia mwaka 2015, Bunge letu lilipitisha sheria kandamizi ambazo zinaminya demokrasia, haki za binadamu, uhuru wa asasi za kiraia kufanya shughuli zao, uhuru wa kujieleza, huru wa kukutana na kutangamana n.k. Baadhi ya sheria hizi ni pamoja na; Sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2019 (Political Parties(Amendment) Act, №1 of 2019), Sheria za matumizi katika chaguzi (Election Expenses Act); Sheria ya habari (Media Service Act); Sheria ya makossa ya kimtandao (Cyber Crime Act); n.k. Sheria hizi zina vipengele vingi ambavyo ama vinampa madaraka makubwa sana Msajili wa Vyama vya Siasa au vinanyima uhuru wa kujieleza.

Baadhi ya vifungu ambayo vilitenguliwa na mahakama ya Afrika Mashariki ni kama kipengele kinachompa mamlaka Msajili wa Vyama vya kusimamia uchaguzi wa ndani ya vyama vya siasa (nomination process) pia kipengele kinachompa madaraka Msajili kusimamia mafunzo yoyote ndani ya vyama.

Hakika ili kuhakikisha kunakuwa na chaguzi huru na zenye kuzingatia haki na kuhakikisha mshindi halali anapata stahili yake kuongoza ni jambo pana lenye kubeba mengi. Ni zaidi ya ile siku moja ya kupiga kura na kuzihesabu kura. Lazima kuhakikisha mazingira mazima yenye kusimamia mzunguko mzima wa kuelekea chaguzi na hadi chaguzi zenyewe zinakuwa katika mifumo na usimamizi bora. Hayo yote yanaweza fikiwa endapo tu kunakuwa na utashi na dhamira ya kweli ya kusimamia haki na usawa. Kutambua na kuheshimu ushindani kwa maana ya kwamba kukubali kuna kushinda na kushindwa. Kukubali kuheshimu matamanio na matakwa ya wananchi na si vinginevyo.

Sisi tunaamini, ili kufikia kuwa na chaguzi zinazoaminika, huru na za haki ni lazima tuanze kwa kuwa na mifumo mizuri ya kisheria unaotupa uwanja sawia wa ushindani wa kisiasa. Tuhakikishe tuna Katiba bora yenye kutoa dira na kusimamia vyema taasisi na mifumo yote pasina kuingiliwa au kushawishiwa kwa namna yoyote iwayo. Tuhakikishe tunazifumua na kuboresha sheria zetu mbalimbali zinazogusa na kuratibu chaguzi zetu. Chaguzi huru na za haki zitalindwa vyema na kusimamiwa kwa kubanwa kikatiba kwa uwepo wa Katiba mpya yenye ubora wa kuhakikisha haki hizi za kisiasa na kiraia zinalindwa, zinapiganiwa na zinatunzwa. Rasimu ya Warioba ilikuwa ni hatua nzuri ya kuelekea katika kupata chaguzi zinazoaminika. Tunaweza kukataa, lakini si kwa hoja bali kwa ubabe. Na ubabe hauwezi kudumu milele .Ni vyema Watanzania tukajiuliza swali moja muhimu sana : Kwa nini watawala wetu na hasa chama tawala katika miaka zaidi ya 40 sasa (vuguvugu la kudai katiba mpya lilianza katika miaka ya themanini), suala la kuandika katiba mpya limekuwa ni kaa la moto ? Sababu hasa ni zipi ?

Tutafakari pamoja.

Ahsanteni.

Wasalam; Michael Dalali na Selemani Rehani

--

--

Michael Dalali

"Truth is an inseparable companion of justice and mercy"-@pontifex| Cogito Ergo Sum| Analyst| Strategist| Facilitator| Translator| Writer & Avid Reader! 🥋