Corpus Christi; Mwili na Damu Takatifu ya Yesu Kristu!
Kanisa kwa namna ya pekee limetenga siku ya kuadhimisha mwili na damu takatifu ya Yesu Kristu ama kwa kilatini Corpus Christi baada tu ya adhimisho la Utatu Mtakatifu. Kwa kutumia siku hii; tunapata fursa kutafakari, kumkiri na kumtangaza Yesu Kristu ndani ya Kanisa na kwa jamii nzima inayotuzunguka. Ni kwa siku hii; Kristu anatembezwa katika jamii yetu kwenye mitaa, njia na kila kona kote duniani kwa shangwe kuu na furaha mithili ya wana wa Israeli walivyotembea na Sanduku la Agano (Rejea: 2 Sam: 12–21).
Kama Sanduku la Agano lilivyokuwa alama na uwepo wa Mungu kwa Waisraeli ndivyo hivyo kwetu sisi sasa ambavyo Ekaristi ni uwepo halisi wa Yesu Kristu katikati yetu.
Kama Sanduku la Agano lilivyokuwa alama ya huruma kwa Waisraeli ambapo kuhani aliingia mara moja katika hema lilipowekwa na kutoa sadaka ya damu ya wanyama kwa ajili ya ondoleo la dhambi, ndivyo basi ilivyo sasa kwetu ambapo Ekaristi Takatifu ni ukamilifu wa huruma ya Mungu kwa wanadamu kwani damu ya Yesu Kristu iliyomwagika msalabani kwa ajili ya ukombozi wetu na yenye kutosha kwa karne zote.
Kama vile ndani ya Sanduku la Agano palivyokuwa na manna ili kuwakumbusha wana wa Israeli upendo mkuu wa Mungu aliowaonesha walipokuwa jangwani, ndivyo hivyo “monstrance” inabeba Ekaristi Takatifu iliyo manna halisi, mkate wa malaika ulioshuka kutoka mbinguni ili kuupa ulimwengu uzima. Mungu mwana aliyekubali kujifanya mwanadamu ili mwanadamu apate kufanywa Mungu.
Ni bahati iliyoje kwetu sisi wanadamu kwa Mungu kukubali kukaa nasi daima na kutushibisha kwa mwili na damu yake kupitia Ekaristi Takatifu. Tumkaribishe basi kwa furaha na shangwe mioyoni mwetu na katika jamii yetu. Tumpe Kristu nafasi atuambie; “… shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako”(Luka.19:5)
Ekaristi (Takatifu) neno ambalo chimbuko lake ni lugha ya kiyunani; eucharistein ikiwa na maana ya kushukuru. Pia “Kanisa” asili na umaana hupatikana kwa kupitia kusanyiko la kiekaristi; kwani Ekaristi huadhimishwa katika kusanyiko la waumini.
Ekaristi Takatifu ni moja kati ya sakramenti saba za Kanisa. Hivyo nayo ni ishara, lakini Ekaristi Takatifu ni uwepo halisi wa Yesu Kristu ndani ya umbo la mkate na divai. Ekaristi Takatifu sio tu ni sakramenti bali pia ni sadaka; sadaka ya kujitoa kwake Kristu mwenyewe kwetu sisi wanadamu. Sadaka ya ukombozi.
Yesu Kristu mwenyewe ndiye kiini cha adhimisho la Ekaristi Takatifu. Yeye mwenyewe (Kristu) ndiye anayeongoza adhimisho lote la Ekaristi bila kuonekana kwa kupitia Padre; ambaye ni Kristu mwenyewe (kwa kilatini, in persona Christi). Katika adhimisho la Misa takatifu padre amejaliwa uwezo maalumu na wa kipekee wa kumwalika mwana wa Mungu ashuke na kuingia katika umbo la mkate na divai na kuwa mwili na damu takatifu ya Yesu Kristu. Ni bahati iliyoje kwa mwanadamu, Padre kujaliwa neema hii ya kipekee kwani hata malaika wa mbinguni hawajapatiwa uwezo huo.
Upekee wa tendo hili la mageuzo (transubstantiation) katika ibada ya Misa Takatifu ambalo ni fumbo la imani si jepesi kwa akili za kibinadamu kulielewa lakini kwa yule ambaye anaamini na kutambua ukuu na uweza wa Mungu hapaswi kutoamini au kuwa na mashaka dhidi ya uwezo wa Mungu kujitoa mwenyewe mwili na damu yake kwa ajili yetu sisi wanadamu.
Na ndiyo maana Mtakatifu padre Pio anapozungumza juu ya umuhimu mkubwa na thamani ya adhimisho la Misa Takatifu anasema; “…endapo watu wangalifahamu kwa kina thamani ya adhimisho la Misa Takatifu, basi ingalihitajika uwepo wa maaskari katika milango ya makanisa ili kusimamia na kuratibu uingiaji katika Kanisa kutokana na kufurika kupita kiasi kwa watu kila iadhimishwapo ibada ya Misa Takatifu”.
Ni katika Alhamisi Kuu; Yesu Kristu mwenyewe ndiye aliweka sakramenti ya Upadre na pia siku hiyo hiyo aliweka pia sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Na alitoa mwito wa kuadhimishwa kwa Ekaristi Takatifu daima; “…nao walipokuwa wakila, alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa, akasema, twaeni; huu ndio mwili wangu. Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote. Akawaambia, hii ndiyo damu yangu ya agano imwagikayo kwa ajili ya wengi…fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu…mimi”. (rejea: Marko 14:22- 25, Luka 22: 17- 20). Ni kwa Ekaristi Takatifu, Yesu Kristu anakaa ndani mwetu, nasi tunakuwa Kristu!
Kama vile ambavyo Yesu Kristu kwa upendo wa kipekee na kwa utayari wake mwenyewe kukubali kujitoa sadaka na kushuka duniani kuja kutukomboa kwa njia ya msalaba pale Kalvari, ndivyo hivyo jambo la kipekee sana kupitia adhimisho la Misa Takatifu, Yesu Kristu anajitoa kwetu sadaka kupitia Ekaristi Takatifu altareni na kutushibisha kwa mwili na damu yake takatifu.
Tofauti ya uwepo wa Yesu Kristu katika matukio hayo mawili ya kipekee; ilikuwa rahisi kwa macho ya kibinadamu kumuona Yesu Kristu msalabani. Licha ya kwamba si wote waliamini katika ukombozi na kujitoa sadaka kwake kama Mungu kumkomboa mwanadamu. Lakini Yesu Kristu amejificha na si rahisi kwa macho ya kibinadamu au imani haba kuweza kuuona uwepo wa Yesu Kristu; mwili na damu katika umbo la mkate na divai.
Daima tunaalikwa kuamini na kusadiki fumbo hili la imani, Mwalimu wa Kanisa, Mtakatifu Thomas wa Akwino katika andiko lake; Summa Theologica anatufundisha na kutufikirisha kwamba endapo Mungu, ambaye ni asili ya vitu vyote (kwa kutamka na vitu vikawa-rejea: Mwanzo 1 pia soma Katekisimu ya Kanisa Katoliki (KKK) 296–298); hivyo ni kwa nguvu na ukuu wa kimungu-Mungu anakuwa katika umbo la mkate na divai. Kwani uwepo wake Mungu si lazima na hautegemei kuwa katika muundo wa kitu; na ndiyo maana tunakiri Mungu yupo mahali popote wakati wowote. Hivyo; haiwezi kuwa shida uwepo wa Mungu katika umbo la mkate na divai. Lakini pia uwepo huo wa Mungu hauzuii muonekano wa mkate kubaki kama mkate na divai kubaki katika muonekano wa divai licha ya uwepo wake (Mungu) lakini uwepo wa mkate si lazima ukawepo uwepo wa Mungu (kabla ya mabadiliko ya kuwa mwili na damu ya Kristu yaani mageuzo; transubstantiation).
Mtakatifu Ambrosi nae akitoa maono yake juu ya mageuzo kwamba; “Muamini kabisa kwamba hiki siyo kile kilichofanywa na maumbile bali kile ambacho baraka imekitakasa. Nguvu ya baraka yapita ile ya maumbile, kwani kwa baraka maumbile yenyewe hujikuta yamebadilika”
Mtakatifu Thomas wa Akwino kwa mara nyingine tena amegusa kwa namna ya pekee na kuipa heshima na hadhi ya juu Ekaristi Takatifu kupitia tungo zake za kusifu sakramenti ya Ekaristi Takatifu; Sakramenti kubwa hiyo au kama inavyofahamika zaidi kwa lugha ya kilatini; Tantum Ergo Sacramentum. Ni kwa kupitia tungo zake hizo tunaona msisitizo wa hitaji wa imani katika kusadiki uwepo wa Yesu Kristu katika umbo la mkate na divai kwani kwa macho ya kibinadamu ni ngumu kumshuhudia Mungu;
“Sakramenti kubwa hiyo,…
yafichikayo machoni, Imani huyaona!
Pia;
“Ninakuabudu kifudi fudi,
Ewe Uungu uliofichika,
Uliye kweli chini ya maumbo haya,
Kwako moyo wangu wote wajinyenyekesha,
Kwa sababu kukutafakari wote,
mzima nashindwa.
Kuona, kugusa, kuonja,
hakukupati wewe,
Kile ambacho chasikika kikisemwa,
chatakiwa kuamini,
Nasadiki kila kitu alichosema,
Mwana wa Mungu,
Hakuna kilicho kweli zaidi,
Kuliko neno hili la kweli
Mtakatifu Fransisko wa Assisi nae anadhirisha upekee na ukuu wa Mungu katika takafari yake ya Yesu Kristu kukubali kushuka na kuingia katika umbo la mkate na divai; “kila mwanadamu na ajawe na hofu, dunia na itetemeke, mbingu na zishangilie na kutoa utukufu wakati Yesu Kristu, mwana wa Mungu aliye hai, anaposhuka kwenye altare katika mikono ya Padre, ni tendo kuu na la ajabu hasa. Unyenyekevu wa ajabu na kujishusha, kwamba Mungu wa dunia, Mungu na mwana wa Mungu, kukubali kujishusha kwa ajili ya ukombozi wetu, yeye mwenyewe amejificha ndani ya umbo la mkate!”
Kama ilivyokuwa vigumu kwa wafuasi wa Yesu Kristu tena mbele yake siku ya Alhamisi Kuu alipowaalika wale mwili na damu yake kuweza kuwaingia akilini na kusadiki; ndivyo bado mpaka sasa hata kwetu sisi waumini wa leo bila imani kuu na neema ya Mungu si rahisi kuona ukuu wa Mungu ndani ya Ekaristi Takatifu.
Ekaristi Takatifu ni chakula cha kiupekee, ni zaidi ya chakula cha manna ambacho Waisraeli walilishwa na Mungu walipokuwa jangwani, lakini chakula chake Yesu Kristu daima chadumu hata uzima wa milele — ukilapo huwezi kupata njaa wala kiu daima; “….Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe. Lakini naliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini” (rejea: Yohane 6: 25–42). “chakula cha kawaida hubadilishwa na kuwa virutubisho vya kutustawisha mwilini lakini kwa Kristu tunapomla; sisi ndiyo tunabadilishwa na kuwa Kristu!” (Mtakatifu Thomas wa Akwino, Summa Theologica)
Na anaongezea zaidi Mtakatifu Thomas wa Akwino fundisho muhimu sana kwamba; “kwa kugawanywa kwa Kristu katika kuumega. mkate; haimgawi Kristu au kumpunguza katika vipande vipande; bali Kristu anabaki yule yule katika umbo la mkate na divai kwa kila yule ambaye anampokea.”
Kwa kupitia mwili na damu ya Yesu Kristu, tunasaidiwa kujitenga mbali na dhambi na kutupa nguvu zaidi ya kupambana na vishawishi.
Katika kumsadiki Mungu na kumkiri mmoja wa wanyang’anyi aliyesulubiwa pamoja na Yesu Kristu pale mlimani Kalvari (Dismas) aliweza kupata uhakika wa ukombozi na kuwa pamoja na Kristu peponi (rejea Luka 23: 39–43). Ndivyo hivyo pia hata leo hii; Mkristu anayeshiriki ibada ya Misa Takatifu anayo fursa adhimu kwa kila inapoinuliwa Ekaristi Takatifu (Yesu Kristu) katika mikono ya Padre huku akitoa mwito na kualika waumini; “…tazama! Mwanakondoo aondoae dhambi za ulimwengu….” kama ilivyokuwa jangwani ambapo Musa alitengeneza nyoka wa shaba na kila aliyemtazama, akaishi (rejea: Hesabu 21:5–9) fursa ya kukabidhi shida, madhaifu yetu, madhambi, maombi yetu na hata shukrani kwake. Ni mwaliko wa kipekee.
Ekaristi Takatifu inatupa nguvu ya kushinda dhambi lakini haituzuii kutokutenda dhambi; kwa sababu utashi wa kutenda au kutotenda dhambi unabaki kwa mwanadamu mwenyewe.
Ekaristi Takatifu ina jambo la kiupekee, la kuweza kuwanufaisha, kupitia sala na maombezi, hata wale ambao hawajaipokea. Mtakatifu Thomas wa Akwino anathibitisha hilo kwa kupitia sala hii; Kumbuka, Mungu, watumishi wako ambao kwao tunakutolea sadaka hii au wanaokutolea sadaka hii ya sifa kwa ajili yao na wengine kutakasa roho zao, kwa tumaini la usalama wao na uongofu. Na tunaona hata Yesu Kristu alipoizungumzia damu yake azizi napo alijumuisha ukombozi kwa wote yaani wenye kumuanini na wasio mwamini kwani aliukomboa ulimwengu mzima pasina mipaka; “damu yangu itakayomwagika kwa ajili yenu na wengi kwa maondoleo ya dhambi….fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi”.
Tunapomtembeza Kristu, katika sherehe ya Corpus Christi, katika jamii yetu tukumbuke kuwa Ekaristi Takatifu ni sakramenti ya upendo na amani. Ni sakramenti ya umoja ambao si tu uthibitisho wa umoja wa Kanisa bali kwa jamii nzima.
Na Michael Dalali
26.05.2018