Je, wananchi wanaweza kupigania katiba mpya?

Michael Dalali
10 min readMar 18, 2022

Na Michael Dalali na Selemani Rehani

Moja ya swali muhimu ambalo limeibuka na kutafakarisha sana ni je, wananchi wenyewe wanaweza kupigania na kuongoza vuguvugu la kutafuta katiba mpya?

Kwa muda wa zaidi ya miongo miwili sasa na zaidi suala la katiba mpya limekuwa likibadilika na kuchukua sura mbalimbali.

Harakati na vuguvugu za kudai katiba mpya zimekuwa zikiendelea toka tuingie katika demokrasia ya vyama vingi mwaka 1992. Mengi yamejadiliwa, lakini kuna masuala mawili muhimu yanahitaji mjadala mpana na tafakuri ya kina.

Msingi wa kuhoji endapo wananchi wanaweza kupigania katiba mpya ni baada ya dalili za hivi karibuni za uwezekano wa ajenda ya kudai katiba mpya ambayo ilikuwa inapambaniwa na kupigiwa upatu na baadhi ya vyama vya siasa hususani vya upinzani kuanza kulegalega katika ajenda hii.

Iwapo wanasiasa wote, wa pande zote mbili wakifikia muafaka kuwa Katiba mpya kwa sasa sio kipaumbele, kama ambavyo chama tawala kimekuwa kikisema, je agenda hii itakufa? Watanzania wanaweza kuibeba na kuimiliki? Na ni kwa namna gani? Haya ni masuala machache ambayo yanatulazimu tuyatafakari kwa kina.

Kama nilivyoeleza awali, moja ya hoja ya chama tawala (Chama Cha Mapinduzi) kupinga suala la dai la katiba mpya limekuwa ni ajenda hii si dai la wananchi bali ni msukumo wa vyama vya kisiasa (upinzani)! Na mara nyingi wamekuwa wakiongeza kuwa wananchi wanahitaji maji, shule, matibabu, miundo mbinu n.k. Wamesisitiza kuwa kwa sasa wanahitaji muda kuimarisha uchumi! Kumekuwa na mazungumzo ya kufanya siasa za kiistarabu na kulinda amani yetu adhimu.

Je ni lini waliwauliza wananchi juu ya suala hili? Ni lini walitafuta maoni ya wananchi kama wanataka katiba mpya au maendeleo? Ni lini chama tawala kilifanya kura za maoni ili kuweza kufahamu takwa la wananchi? Wangetueleza hili kwa takwimu, ingetusaidia sana. Yaani asilimia ngapi ya wananchi wanahitaji wanasema katiba sio muhimu.

Ni maoni yetu kuwa, hata kama ni kweli kuwa wananchi hawataki katiba mpya, je tumewahi kujiuliza kwa nini hawataki katiba mpya? Je kama ni kweli si jambo la kuibua hamasa kutamani kujua zaidi sababu hasa inayopelekea wananchi wasione katiba mpya kama suala la kipaumbele na la kupewa uzito wa hali ya juu ? Je, ina maana wananchi hawataki, mathalani: kushiriki katika kuunda katiba yao, hawataki tuwe na mihimili iliyo huru, inayochungana na haingiliani; hawataki kuwa na uhuru wa kuomba kuchaguliwa na wananchi wenzao katika nafasi mbalimbali za uongozi bila kulazimishwa kujiunga na chama cha siasa; hawataki maadili ya viongozi; hawataki tuwe na Tume huru ya uchaguzi; Hawataki ushirikishwaji, kuimarisha uwazi, demokrasia, utawala wa sheria, uwajibikaji na kuheshimu haki za binadamu. Yote haya hawayataki?! Masuala haya ndio msingi wa kuinua uchumi. Kama hawayataki yote haya wataweza vipi kuondokana na umaskini?

*Kibonzo shukrani kwa Kingo!

Tukumbuke maneno ya Rais mstaafu wa awamu ya nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete aliyosema 21 Machi, 2014 akizindua bunge la katiba alibainisha kwa mapana tija ya katiba mpya, sifa zake, na zaidi umuhimu wake kwa taifa letu. Kwa maneno yake alisema ; “ ….ni matarajio ya watanzania mtatunga katiba itakayokubalika na wengi (makofi), katiba inayotekelezeka, katiba itakayoimarisha muungano wetu kwa kuondoa changamoto za muungano za sasa (makofi na vigelegele), katiba inayotupa mfumo bora wa kuongoza na kuendesha mambo yetu, katiba itakayoimarisha upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Tanzania licha ya tofauti zao za asili kwa upande wa muungano na maeneo wanakotoka na tofauti za jinsia, rangi, kabila, dini na ufuasi wa vyama vya siasa. Katiba itakayo dumisha amani na usalama wa nchi yetu. Katiba itakayostawisha zaidi demokrasia, kuheshimu haki za binadamu, utawala wa sheria, utawala bora na kudhibiti maovu. Na mwisho ingawaje sio mwisho kwa umuhimu, katiba itakayoweka mazingira mazuri kwa uchumi wa nchi yetu kukua na wananchi wote kunufaika sawia na maendeleo yatakayopatikana ”.

Na iwapo haya yote hawayataki basi kama jamii tuna tatizo mahali na hatuna budi kukaa chini na kujiuliza tumekosea wapi. Aidha kama wananchi hawataki katiba mpya, je chama tawala hakioni kuwa kina wajibu wa kuonyesha uongozi kwa kuwahamisha na wananchi na kuwajengea uwezo waelewe umuhimu wa katiba mpya?

Zipo nyakati katika historia yetu, chama tawala (CCM) kimewahi onyesha dira kwa kufanya maamuzi magumu ambayo wengi walikuwa na mtizamo tofauti mathalani maamuzi ya kuacha mfumo wa chama kimoja na kuingia katika mfumo wa vyama vingi mnamo mwaka 1992. Ikumbukwe kitakwimu, wananchi takribani asilimia themanini hawakutaka nchi iingie katika mfumo wa vyama vingi huku asilimia ishirini tu ndiyo ilitaka kuingia mfumo wa vyama vingi. Lakini busara, hekima na uongozi wa chama tawala (CCM) uliona ni jambo la kheri kuamua hata kama si jambo lenye kuungwa mkono na wengi ila nchi iingie katika mfumo wa vyama vingi kwa faida lukuki sambamba na wakati kuwa unataka uamuzi huo.

Hivyo hata hili la kuhakikisha nchi inapata katiba mpya kwa maslahi mapana ya nchi halitakuwa jambo la kwanza kutendwa na chama tawala, endapo dhamira na maamuzi thabiti yakiwepo.

Lakini pia, kwa kuhakikisha katiba mpya inapatikana, CCM itakuwa inaenzi na kuheshimu kauli zake. CCM itakuwa inawaenzi viongozi wake kama Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na pia Rais wa awamu ya tano, Hayati John Pombe Magufuli ambaye nae kwa kinywa chake alipata ahidi wakati akizindua Bunge, 20 Novemba 2015 kwamba ; “ Serikali yangu imepokea kiporo cha mchakato wa Katiba ambao haukuweza kukamilika katika awamu iliyopita kutokana na kutokamilika kwa wakati kwa zoezi la uandikishwaji la wapiga kura. Napenda kuwahakikishia kuwa tunatambua na kuthamini kazi kubwa ya kizalendo iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya ukusanyaji wa maoni kuhusu katiba mpya, Tume ya marekebisho ya Katiba na Bunge la Katiba lililotupatia Katiba Inayopendekezwa tutatekeleza wajibu wetu kama ilivyoainishwa katika sheria ya marekebisho ya katiba”.

Katiba ni watu na watu ni katiba. Ndio mfumo wa maisha yetu. Ni mkataba wa viongozi na wananchi. Katiba bora ni maendeleo.

Tuzitazame tena hoja hizi kwa umakini mkubwa. Kifalsafa na hasa kimantiki (logic) kuna hoja kadhaa, mathalani: Je vyama vya kisiasa ni sehemu ya wananchi? au je, kama si hoja ya wananchi (ambao hata kwa uchache wao wamo katika vyama vya siasa) je haina tija kuhitajika kuwepo? Je vyama vya siasa vinabeba maono ya nani? Na iwapo havibebi maono ya wananchi, je hivyo ni vyama vya siasa? Iwapo vyama vya siasa vinapuuza matarajio na maono ya wananchi, je vina umuhimu wowote wa kuendelea kuwepo?

Mawazo na matamanio ya wananchi lazima yabebwe na taasisi (vyombo) mbalimbali katika jamii kama vile vyama vya siasa, asasi za kiraia, vyombo vya kitaaluma, vyama vya ushirika, vyombo vya habari. Taasisi hizi kama vyama vya siasa, asasi za kiraia, vyombo vya habari nk ni vyombo ambayo vinawaunganisha wananchi, ni sauti ya wananchi, pia vinatoa uratibu katika kuwawezesha wananchi kufikia shabaha zao. Matamanio na madai ya wananchi mara kwa mara hubebwa na kupiganiwa na taasisi zenye viongozi walio na dira na shupavu.

Kwenye sayansi ya siasa, kazi kubwa vyombo hivi (yaani vyama vya siasa, vyombo vya habari na asasi za kiraia) huitwa “ interest articulation” and “interest aggregation ”. Yaani uwezo wa taasisi (vyombo) hivi kuchambua kwa kina nakuelewa maslahi ya makundi tofauti ya jamii kwa ujumla ni muhimu kufahamu kama watanzania wanahitaji katiba mpya. Na kwa interests aggregation ni ule umuhimu wa kutafuta mizania baina ya maslahi tofauti ya watu ili kufahamu kama katiba mpya ni kipaumbele cha watanzania. Kazi hii inalegalega!

Kwa uhalisia, nguvu na uungwaji mkono mkubwa wa taasisi au vyama vya namna hii iliyoelezwa katika aya iliyotangulia huja tu endapo wanasimama katika ajenda ya wananchi au kile wananchi wanachotaka. Vyama hivi kufifia au kudorora au hata kupotea kabisa kwenye ramani yake pale tu wananchi wakiona kabisa vimekoma kuwa sauti yao.

Sasa mkwamo na kiu ya wananchi huingia shubiri endapo vyombo, vyama au taasisi hizi zikikoma kuwa sauti yao na kuwa wawakilishi wa kupigania ajenda zao.

Tukirudi katika suala la katiba mpya, nchini Tanzania wananchi kwa miaka nenda rudi wamekuwa na tamanio hili la kupata katiba mpya ambayo itakuwa chimbuko toka kwao na lenye kubeba matarajio, maono, matamanio na matakwa yao. Kwa kutambua hili Rais wa awamu ya nne Mheshimiwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliwaahidi Watanzania pale aliposema ; watanzania watakuwa na katiba mpya ifikayo mwaka 2014 ! Tukashuhudia kuanza kwa mchakato rasmi mwaka 2011 kwa kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 83/2011 na baadaye ikatungwa Sheria nyingine ya Kura ya Maoni Na. 11/2013, kuundwa kwa Tume ya Katiba chini ya Jaji Mstaafu Joseph Warioba, na hata Bunge Maalumu la Katiba (Constituent Assembly).

Bado tamanio lao hili la kupata Katiba mpya halijafanikiwa, hivyo linaendelea na litaendelea kuwa ajenda na dai la wananchi. Na yeyote ambaye atamudu kulipigania basi atapata uhakika wa uungwaji mkono na wananchi. Hapa iwe asasi za kiraia, chombo cha habari, taasisi za kitaaluma, au hata chama cha siasa nk.

Tukirudi nyuma kidogo katika historia ya nchi yetu, miaka ya mwishoni mwa themanini na mwanzoni kwa tisini, Tanzania ilipitia vuguvugu la kudai katiba mpya. Vuguvugu hili kutokana na hali ya kisiasa na kisheria kwa wakati huo (nchi kuwa katika mfumo wa chama kimoja), vuguvugu ilibidi libebwe kwa kuundwa kwa Kamati ya Kudai Katiba Mpya (wakati huo katiba ilipiga marufuku kuanzisha chama kingine cha siasa) ambayo ilizunguka kuelimisha wananchi, kusikia wananchi, kufanya makongamano na kushirikisha tathmini mbalimbali. Vuguvugu hili liliongozwa na wananchi ikiwemo watu wa taaluma mbalimbali mathalani wanasheria, wasomi wa fani mbalimbali, wanazuoni, lakini pia walikuwepo wanasiasa.

Baadhi ya wanasiasa na wazee waliokuwa mstari wa mbele katika kudai katiba mpya ili iruhusu mfumo wa vyama vingi ni kama vile marehemu Bob Makani, Mzee Fundikira, Kasela Bantu, James Mapalala, Simon Kashura na wengine wengi wao ni marehemu hivi sasa. Wazee hawa walianzisha kamati za kudai mabadiliko ya katiba ili kuruhusu mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi.

Kwa wasomaji wa kizazi kipya wanaweza kusaka machapisho kama ; “ Towards Multiparty Politics in Tanzania” (Kuelekea mfumo wa siasa ya vyama vingi nchini Tanzania) chenye makala za wanazuoni kama marehemu Profesa Max Mmuya, Profesa Chaliga, Profesa Haroub Othman n.k. ambao waliangalia kwa kina harakati za kudai katiba mpya katika kipindi kile cha mwanzoni mwa miaka ya tisini. Kuna mafunzo lukuki ya kuchota.

Kamati hiyo ndiyo baadae ilikuja kuzaa na kurasimishwa kwa kile kilichokuja kuwa chama cha siasa, yaani National Convention for Construction Reforms-Mageuzi ama kwa kifupi NCCR-Mageuzi.

Hapa napo kuna jambo la kuhoji na funzo ndani yake. Je, kwa ajenda hii na kamati ile ambayo ilikuwa inapigania kuja kubadilika na kuzaa chama cha siasa ilikuwa na tija ? je tija ingepatikana zaidi na kuwa endelevu endapo kisingebadilishwa na kuwa chama cha kisiasa ?

Baada ya hapo na yaliyojiri, vuguvugu la kudai katiba mpya na hasa tamanio la wananchi lilififia. Hii nina uhakika haina maana suala hili lilikoma kuwa tamanio au hitaji la wananchi, la hasha. Na ndiyo maana limekuwa linaibuka miaka na miaka.

Kuanzia 2010 vuguvugu hili lilianza tena kwa sura nyingine. Tukashuhudia asasi za kiraia nazo kuwa mstari wa mbele, ndipo tukaona asasi mathalani Jukwaa la Katiba na AZAKI nyingine zikijikita kuelimisha na kufanya kufanya kazi kubwa kwenye eneo hili la Katiba mpya. Sambamba pia vyombo vya habari na vyama vya siasa navyo havikuwa nyuma katika mapambano haya.

Mapambano haya yaliendeshwa hadi kukawa na Rasimu ya Katiba ya Tume ya Katiba chini ya Jaji Mstaafu Warioba na kuwa na Rasimu ya Katiba ya Bunge Maalumu la Katiba chini ya Hayati Samuel Sitta (Katiba Inayopendekezwa). Lakini napo tukaingia katika mkwamo.

Hapa kwa mara nyingine tunapashwa kuhoji na kujihoji, je taasisi ambazo zilikuwa zinaongoza wananchi katika kusaka katiba mpya ziliwatendea haki wananchi au ziliweka mbele maslahi yao na ajenda zao ndani ya ajenda mama ya katiba mpya ? Je, kwanini asasi hizi zilikoma kuendelea kuendesha miradi na programu mbalimbali juu ya Katiba mpya ? Je, vyombo vya habari ambavyo vilitenga muda kuelimisha na kuwa na mijadala katika katiba mpya- kwanini viliacha ? Je, wananchi walikuwa na fursa ya kuendesha mapambano haya kwa namna nyingine ili kufikia dhumuni kuu la kupata katiba mpya ? kuna funzo gani katika haya ?

Katika kipindi cha 2015–2022 ; Safari ya kudai katiba mpya ilichukua taswira mpya kwa vuguvugu la kudai katiba mpya kuanza tena kuibuka na kuongozwa na vyama vya siasa hususan vya upinzani na kwa upekee Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Hapa labda tukikumbusha kidogo, Uchaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ulifungua ukurasa mwingine toka wananchi na kwa vyama vya siasa kwa namna chaguzi hizo mbili zilivyoacha gumzo kuu na hofu juu ya namna gani chaguzi zetu zinaendeshwa na kuratibiwa, na zaidi kama hata zinajali na kuzingatia tamanio la wananchi juu ya viongozi wanaowataka kushika nyadhifa mbalimbali. Hapa suluhu na faraja kuu ya shubiri yote ilionekana ni uwepo wa Katiba mpya tu na si vinginevyo!

Kwa kuangalia kwa ukaribu, bila kuzama kwa kina kwenye visababishi vya matukio hayo tunaona jitihada hizi zilizokuwa zinaongozwa na vyama vya upinzani zimekuwa zikigonga mwamba na kulazimika kusimama. Ambapo msingi mkuu wa kufaulu kupata katiba mpya kuendelea kudorora.

Ni muhimu tujikumbushe kwamba, vyama vya siasa mathalani chama tawala (CCM) na chama kikuu cha upinzani nchini (CHADEMA) vyote kwa pamoja vilipata kuahidi na kubainisha suala la katiba mpya katika ilani zao za uchaguzi mkuu 2015. CCM katika Ilani ya mwaka 2015 ukurasa 189 Kifungu cha 144 (e), iliahidi kukamilisha mchakato wa katiba mpya huku CHADEMA katika Ilani zake za toka mwaka 2010, 2015 na 2020 imekuwa inaahidi kuanzisha mchakato wa kuandika katiba mpya ndani ya siku 100.

Kama mwanzo wa makala haya, gumzo la fikra ya je wananchi wanaweza kuendesha mapambano yao wenyewe bila utegemezi wa taasisi kama vyama vya siasa limeibuka tena kwani matukio ya kisiasa yamekuwa (kama ilivyokuwa awali) yakiathiri mapambano haya. Kwa sasa, tumeona maendeleo na matukio ya kisiasa kwa baadhi ya vyama vya upinzani imepelekea kwa baadhi ya viongozi waandamizi kuibuka na kauli zenye kuacha shaka na maswali juu ya hatma ya kuongoza kwa msimamo thabiti na mstari wa mbele mapambano ya kudai katiba mpya.

*Kibonzo shukrani kwa Kingo!

Fikira tu ya kurudi nyuma kwa taasisi hizi za kisiasa, kumegusa na kushtua mioyo ya wananchi ambapo wengi walikuwa nyuma ya ajenda mama ya hitaji la katiba mpya. Wengi wanaona kuachwa au kurudi nyuma katika suala hili inafifisha mapambano haya. Lakini wapo pia wanaona vyama hivi vya kisiasa vinasaliti ajenda za wananchi (kama ajenda ya Katiba mpya) pundi ajenda na maslahi yao ya kisiasa yakitimia.

Sisi wananchi tunapaswa kuendelea kujihoji, je tunaweza kupigania matakwa yetu na ajenda tunazozitaka ? tunaweza kupigania kupata katiba mpya bila utegemezi wa vyama vya siasa, asasi za kiraia, vyombo vya habari ? mapambano hayo tuyaongozaje ?

Je wananchi wanaweza kumiliki na kuendesha vuguvugu la kudai katiba mpya ?

--

--

Michael Dalali

"Truth is an inseparable companion of justice and mercy"-@pontifex| Cogito Ergo Sum| Analyst| Strategist| Facilitator| Translator| Writer & Avid Reader! 🥋