Jumuiya Ndogondogo: mwiba kwa wakatoliki?

Michael Dalali
5 min readOct 11, 2022

Kanisa la Kisinodi; Ushirika, Ushiriki na Umisionari !

Salamu hii ya kipindi cha Sinodi, inatukumbusha juu ya Kanisa letu Katoliki na wajibu wa kila mbatizwa hasa katika mambo makuu matatu yaani ; Ushirika, Ushiriki na Umisionari. Mambo haya matatu yanaungana na kudhihirishwa katika namna Kanisa letu Katoliki linajiendesha ikiwemo uwepo wa Jumuiya Ndogondogo. Ni katika Jumuiya Ndogondogo ndipo waumini wakatoliki wa eneo husika angalau wastani wa kaya nane (8) hadi kumi na nne (14) hujumuika kila wiki kuja kusali kwa pamoja, kujuliana hali na kushiriki katika mipango ya kulitegemeza kanisa kiroho na kitaasisi.

Lakini ni ukweli mchungu, Jumuiya Ndogondogo zimekuwa mwiba kwa baadhi ya wakatoliki. Baadhi wanazichukia, wanaona ni usumbufu, wanaona ni urasimu katika kupata masakramenti na malalamiko mengine mengi. Ni afya kwa waumini kutafakari kwanini hali hii na labda kuja na mapendekezo au maboresho yenye tija. Lakini sambamba na kuziangalia Jumuiya Ndogondogo, iwe fursa pia kufanya tafakari binafsi na kuitathmini nafsi na mwenendo wako binafsi kama Mkatoliki hai na mbatizwa.

Miongoni mwa sababu dhidi ya kuchukiwa kwa jumuiya ni viongozi wa jumuiya kuwa ‘wanoko’ (wenye kufuatilia kwa ukaribu) juu ya mwenendo wa mahudhurio ya wanajumuiya ndogondogo. Mfano : Jumuiya Ndogondogo imekubaliana kusali kila jumamosi asubuhi. Wanajumuiya wanakwepa kuhudhuria na mahudhurio yanakuwa hafifu jambo ambalo linahatarisha uhai wa jumuiya. Hapa muumini anapashwa ajitathmini kabla ya kuwa mkali kwamba viongozi wanafatilia kwa ukaribu mwenendo wa mahudhurio — anapashwa ajiulize kwanini amekuwa mlegevu kwenda kusali na majirani zake wakatoliki ? Ajiulize endapo kila mmoja angekwepa kwenda kusali je jumuiya ingekuwepo ?

Kama ni dharura za majukumu ya kikazi ; basi ni muhimu kuwasilisha hayo kwa viongozi wake huku akijitahidi hata mara moja kwa mwezi au kwa kadiri atakavyoweza kutenga muda angalau wa kuungana na wengine na kusali jumuiya. Sambamba na kuhamasisha wanakaya yake kushiriki kwa wingi kuwakilisha kaya husika.

Sababu hii ya mahudhurio hafifu imekuwa pia kichocheo na sababu nyingine ya jumuiya kuwa mwiba kwa baadhi ya wakatoliki hasa pale ambapo wao au wanakaya zao wanapokuwa na uhitaji wa masakramenti. Kwa utaratibu wa parokia nyingi, kumekuwa na mfumo wa kupata mrejesho wa mwenendo wa mkristu katika ngazi ya chini kabisa yaani namna anavyoshiriki katika jumuiya. Fomu hizi sambamba na kuwapa fursa viongozi kutoa maelezo juu ya mwenendo wa mkristu pia inaweka bayana hata namna ambavyo anatekeleza wajibu wake mathalani rekodi zake za utoaji wa zaka.

Hapa kwa wale ambao wana mahudhurio mazuri au wajitahidi kutekeleza takwa la utoaji wa zaka huwa hakuna changamoto sana. Lakini hugeuka shubiri pale ambapo mwanajumuiya anakuwa mlegevu asiye shirikiana na wakatoliki wenzake katika sala za jumuiya. Inakuwa ngumu ajaziwe nini pale muumini huyo huwa hatoi zaka na hana rekodi zozote.

Kiongozi ambaye anasimamia kweli kwa kuweka bayana mwenendo usioridhisha wa ushiriki sambamba na kutokushiriki kwake katika matoleo ya zaka ni rahisi kugeuka mbaya mbele ya macho ya muumini wa namna hii pasina kujali kwamba yeye muumini ndiye chanzo yote.

Wapo ambao huzilalamikia jumuiya kuwa na mlolongo mwingi wa michango. Malalamiko haya huwepo pia kwa ngazi ya Parokia, kwamba Kanisa hivi sasa limekuwa na michango mingi sana. Hapa kuna kazi kubwa bado ya kufanywa kujaribu kuinjilisha na kugusa mioyo ya watu katika utoaji na kulitegemeza Kanisa hasa kwa zama za sasa ambazo hakuna tena misaada toka nje ya nchi. Kanisa la sasa (“Kanisa la Afrika”) linajitegemeza lenyewe kupitia waumini wake wenyewe.

Michango ambayo ipo katika jumuiya huwa inaanzia juu kabisa katika mipango na mahitaji ya Kijimbo na/au Kiparokia. Hivyo basi, jumuiya ni watekelezaji tu wa mipango ya Parokia au/na Jimbo.

Pia, ni imani yangu kwamba hakuna Paroko au Askofu hatomruhusu muumini asishiriki sala na sakramenti mbalimbali kwasababu tu hajakamilisha kutoa Tegemeza Parokia au Tegemeza Jimbo au mchango wa UWAKA au mchango wa WAWATA nk.

Ni muhimu sana muumini kuona anao wajibu wa kulitegemeza na kuliimarisha Kanisa lake kwa michango yake kadiri ambavyo anabarikiwa na Mungu. Muumini ajue kwa kufanya hivi anakuwa anatekeleza amri ya Kanisa — Amri ya tano ; “Saidia Kanisa Katoliki kwa zaka, (sadaka na michango mbalimbali)”.

Muumini anapashwa awe na amani kabisa na asione aibu kushiriki endapo ana kipato duni ambacho kinapelekea yeye kutoa kwake ni kiwango cha chini ; awe huru atoe kile alichobarikiwa hata kama ni kidogo. Kinachopashwa tu ; ajitoe kwa ajili ya Mungu kwa moyo wote bila kujibakiza. Awe kama mjane maskini aliyetoa sarafu mbili na Bwana wetu, Yesu Kristu alimthibitisha kuwa amejitoa zaidi kuliko hata matajiri waliokuwa wametoa fedha nyingi ; “Ninawaambia hakika, huyu mjane ametoa zaidi kuliko wote! 44 Wengine wote wametoa kutokana na ziada ya mali zao; lakini huyu mama ingawa ni fukara, ameweka kila kitu alichokuwa nacho, hata na kile alicho hitaji kwa ajili ya riziki yake.” (Rejea Marko 12 : 41–44).

Makwazo ndani ya ubinadamu wa viongozi wa kikanisa; hii ni moja pia ya sababu tajwa ambapo baadhi ya waumini wanarudi nyuma kushiriki katika sala za jumuiya ndogondogo. Viongozi ambao hawana mwenendo mzuri mathalani ulevi wa kupindukia, uzinzi, visasi, na mengine mengi huwa makwazo kwa waumini.

Wapo baadhi ya wanajumuiya wanakuwa wanakwepa au kuacha kwenda kusali nyumba fulani ambayo hawana mahusiano mazuri — wana magomvi binafsi yao. Au wapo pia waumini ambao wanakuwa hawasali au kutokutoa ushirikiano mzuri pale muumini amechaguliwa katika uongozi wa jumuiya ndogondogo kwasababu tu wana magomvi binafsi au magomvi ya kiukoo au wengine wana magomvi ya mipaka. Hapa ni vizuri sana kukumbuka namna sisi tunaomfuasa Kristu namna ambavyo tunaaswa kuwa wepesi kusamehe hata saba mara sabini (Rejea : Mt 18: 21–35), na zaidi kuwapenda adui zetu (Rejea : Mathayo 5: 43–48). Lakini endapo ukashindwa kabisa hayo yote — basi ujitahidi kuwa na ukomavu wa kutenganisha kati ya magomvi binafsi na kuangalia ustawi wa Kanisa ambalo si sehemu ya magomvi hayo.

Basi ni busara kwa waumini kuona namna bora ya kuwasahihisha viongozi walei hawa wa jumuiya. Endapo njia mbalimbali za kuwasahihisha zinapogonga mwamba basi kwa hekima kuwasilisha suala hilo katika ngazi za juu za Parokia kuanzia viongozi wa Kanda husika na hata kufikisha kwa Halmashauri ya Walei au kwa Paroko kwa ushauri na maamuzi mengine.

Lakini katika hili, waumini wote tunaalikwa tusiache kuwaombea hawa ambao madhaifu na dhambi zao hujitangaza hadharani ili warejee katika uongofu. Tujiepushe kuwa sehemu ya kutangaza madhaifu na maanguko ya wenzetu.

Wakatoliki tunapashwa kuzipenda jumuiya ndogondogo zetu. Tunapashwa kuona ni fursa ya kipekee Kanisa imetupa kuweza kukutana kama Kanisa katika maeneo yetu na kuungana kwa pamoja katika sala na shukrani zetu.

Jumuiya inapashwa iwe chachu ya upendo, umoja na mshikamano. Inatuleta karibu watu ambao tunaishi sehemu moja wenye imani sawa. Hivyo jumuiya inapaswa iwe kimbilio la kuleta unganiko wa kidugu katika Kristu.

Tuzitumie Jumuiya ndogondogo kama mahala pa kutujenga zaidi kiroho kuanzia watoto wetu kwa kuwapa fursa kushiriki na kuwa na walimu wa imani katika jumuiya ambao watawafundisha. Kila mwanajumuiya awe mstari wa mbele kushiriki katika kushirikisha wanajumuiya wengine katika tafakari na mang’amuzi yake juu ya masomo ambayo yanasomwa katika jumuiya na si kuwaachia baadhi ya waumini au viongozi kutoa tafakari.

Jumuiya iwe ishara na kichocheo cha amani na furaha katika familia zetu. Pale ambapo jumuiya inakutana kusali. Msalaba na visakramenti vinginevyo kama sanamu ya Mama Bikira Maria au Mtakatifu somo wa Jumuiya husika anafika katika kaya yako ; alete baraka, maelewano, furaha ndani ya nyumba. Awe chanzo cha utatuzi wa migogoro ya kifamilia na kurejesha amani baina ya wanandoa, kurejesha amani baina ya watoto, kurejesha amani baina ya waumini na Kanisa lao.

Kila mbatizwa anao wajibu mkubwa wa kulijenga na kuliimarisha Kanisa Katoliki na kwa kujitoa na kushiriki kikamilifu anakuwa kweli Mmisionari. Anakuwa ameshiriki umoja wa Kanisa Katoliki. Amekuwa sehemu ya ukombozi wa Kristu wa Msalaba ambaye alipokea jukumu la ukombozi pasina kulikimbia au kutoa sababu au kasoro.

Kanisa la Kisinodi ; Ushirika, Ushiriki na Umisionari !

--

--

Michael Dalali

"Truth is an inseparable companion of justice and mercy"-@pontifex| Cogito Ergo Sum| Analyst| Strategist| Facilitator| Translator| Writer & Avid Reader! 🥋