Katiba “ya viraka vya kisiasa”!

Michael Dalali
7 min readMar 30, 2022

Na Michael Dalali na Selemani Rehani

Tanzania ni taifa ambalo limeshakomaa kwa kuwa na zaidi ya miaka sitini (60) toka kupata uhuru wake. Tangu kupata uhuru miongoni mwa mambo ambayo Tanzania ilirithi toka kwa Mkoloni na kuendelea nayo ni pamoja na Katiba. Taifa jipya, huru na la kizalendo: — Tanzania halijawahi kuwapa fursa wananchi wake kushiriki katika kutunga katiba yao na kuwa na Katiba yao wenyewe wanayoitaka, ambayo inatokana na watu na kwa ajili ya watu. Ili kuielewa hili vyema ni muhimu sana tukaelewa historia na mabadiliko ya katiba yetu.

Katiba ya sasa ya mwaka 1977 imepitia maboresho kumi na nne lakini bado ina mapungufu mengi nahaijakidhi kiu ya Watanzania walio wengi. Kwa lugha ya picha tunaweza sema ni uwekwaji wa “viraka” mithili viraka viwekwavyo katika nguo kuu kuu. Hapa tunaweza kuona umuhimu wa kuwashirikisha na kuwapa nafasi wananchi kutoa mawazo yao (yaani consultation).

*Kibonzo shukrani kwa Kingo

Hebu tutizame kwa kina na kujikumbusha maboresho hayo makubwa na madogo ambayo Katiba hii imekwisha yapitia mpaka sasa;

Mwaka 1961, tulirithi Katiba ya mkoloni, hii iliitwa Katiba ya Uhuru (Independence Constitution). Katiba hii ilikuwa na mfumo wa Westminster ilimtambua Malkia wa Uingereza kama mtawala mkuu wa nchi (yaani Head of State). Huku tukiwa na Waziri Mkuu kama mtendaji mkuu wa Serikali (yaani Head of Government). Kwa hiyo tulirithi katiba ya mkoloni ambayo ilitungwa kwa ajili ya kendeleza utawala wa kikoloni.

Mwaka 1962, ikiwa ni mwaka mmoja tu baada ya kupata uhuru tulipata katiba ya Jamhuri ya Tanganyika. Hii ilikuwa ni baada ya kufanyika mabadiliko ya msingi sana ya kiserikali na kiutawala ambapo Tanganyika ikawa jamhuri kamili hivyo Malkia wa Uingereza alikoma kuwa Mkuu wa Nchi, na Jamhuri ya Tanganyika ikawa na Rais ambaye akawa ni Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu. Huu ndio ulikuwa mwanzo wa kumrundikia mamlaka mengi Rais. Kama wataalamu wa katiba wanavyobainisha, huu ndio ulikuwa mwanzo wa kuwa ‘Imperial President’ yaani Urais wa Kifalme.

Ifahamike, mabadiliko haya ya katiba hayakufuata taratibu za kawaida hususan ushirikishwaji wa umma kwani wabunge 71 wa TANU walijigeuza na kuwa Bunge Maalumu la Kutunga Katiba na kupitisha mabadiliko bila kuwashirikisha wananchi.

Badiliko jingine kubwa lilikuja mwaka 1964 baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kuwa nchi mbili huru yaani Zanzibar na Tanganyika ziliungana na kuzaliwa Tanzania, ilikuwa ni lazima kufanyika mabadiliko ya katiba ili kuweza kukidhi mazingira mapya ya muundo mzuri wa serikali. Mabadiliko haya pia yalifanywa bila kushirikisha wananchi kwa ujumla wake.

Mabadiliko haya yalifuatiwa na mabadiliko mengine ya katiba ya muda ya mwaka 1965 (the Interim Constitution of Tanzania). Mabadiliko haya yalipiga marufuku vyama vya upinzani na kuruhusu shughuli za siasa zifanywe na vyama vilivyopo madarakani tu ambavyo vilikuwa ni chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kwa upande wa Tanzania Bara na chama cha Afro Shirazi Party (ASP) kwa upande wa Tanzania Visiwani (Zanzibar). Vyama vingine vya upinzani vilisitishwa kwa lengo la kuimarisha umoja na mshikamano wa taifa. Hivyo basi tukaingia katika mfumo wa chama kimoja katika kila pande ya muungano sambamba na zama za chama kushika hatamu. Mabadiliko haya pia yalifanywa bila kushirikisha wananchi kwa ujumla wake.

Mwaka 1977 tukafanya mabadiliko mengine ya katiba ambayo yamedumu hadi sasa. Ilikuwaje? Wajumbe 20 waliteuliwa kuandaa katiba hii, kumi kutoka Bara na kumi kutoka Zanzibar. Tume hii iliongozwa na Marehemu Sheikh Thabit Kombo akisaidiwa na Mzee Pius Msekwa kama Katibu wa Tume. Ni vyema tukakumbuka kuwa tume hii ni ile ile iliyotunga katiba iliyopelekea kuundwa kwa CCM.

Katiba hii ya mwaka 1997 ilipitishwa ndani ya masaa matatu na Bunge maalumu lililoteuliwa na Rais kutokana na Bunge la kawaida. Hapa tena tunaona kutokushirikishwa kwa Watanzania kwa ujumla wao katika kutunga katiba yao.

Labda vijana waliozaliwa kuanzia miaka ya tisini mpaka leo wanaweza kuhoji kwanini vyama viwili vya kisiasa kuungana kwao kuathiri hadi Katiba ya nchi?

Ifahamike kuwa kwa wakati huo, Kikatiba Tanzania ilikuwa chini ya mfumo wa chama kimoja tofauti na ilivyo sasa ambapo kikatiba nchi ipo katika mfumo wa vyama vingi. Hivyo badiliko hilo lilikuwa na athari kubwa katika mfumo wa kisiasa na kiserikali hata kupelekea uwepo wa hitaji la mabadiliko katika Katiba.

Kama tulivyotanabaisha hapo awali, baada ya maboresho makubwa matatu, Katiba yetu ilipitia maboresho mengine madogo madogo kadiri ya mahitaji na nyakati mbali mbali. Hebu tujikumbushe maboresho hayo madogo madogo ambayo hasa yalikuwa ni mabadiliko katika vifungu vya katiba;

Mwaka 1979 mabadiliko ya kuanzishwa kwa mahakama ya rufaa ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania yenye mamlaka katika pande zote mbili za muungano.

Faida za Muungano zilienda sambamba na changamoto zake ambapo mnamo mwaka 1980 ilibidi kufanyike mabadiliko katika katiba yaliyolenga kutatua kero za muungano hasa kwa upande wa Zanzibar ambapo kwa wakati huo kuliibuka vuguvugu la kudai uhitaji wa mabadiliko na kutaka kuwepo Serikali tatu. Dai hili liliongozwa na Rais wa Zanzibar kwa wakati huo, Aboud Jumbe.

Mwaka 1982 badiliko au “kiraka” kingine kiliwekwa katika Katiba yetu ambapo kusudi kubwa ilikuwa ni katika kuboresha taratibu za kuteua wakuu wa mikoa na wilaya.

Mwaka 1984 kwa kuzingatia Tamko la Haki za Binadamu la mwaka 1984 Katiba yetu ilifanyiwa maboresho madogo kuweza kugusa na kuzingatia haki za binadamu.

Vuguvugu la kudai vyama vingi ambalo lilianza miaka ya themanini kuelekea mwanzoni mwa mwaka tisini, lilipelekea kupitishwa uamuzi wa kuanzisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kusimamia chaguzi na hasa ikilenga kuja kuratibu na kusimamia vyema chaguzi katika mfumo mpya wa vyama vingi kwani kabla ya hapo chaguzi zilikuwa zinasimamiwa na chama tawala chenyewe. Hivyo, mwaka 1990 Katiba ikafanyiwa maboresho na kuzingatia uanzishwaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Sambamba na mabadiliko ya kuiweka Tume ya Uchaguzi (NEC) katika Katiba, pia mwaka 1990 kulifanyika mabadiliko mengine madogo kwenye Katiba ambayo yaliweka utaratibu wa kuwa na mgombea mmoja wa Urais upande za Zanzibar ili kuondoa utaratibu wa awali ambao ulilalamikiwa.

Mwaka 1992 kulifanyika mabadiliko madogo ya katiba kurejesha kwa mara nyingine tena mfumo wa vyama vingi nchini na kuweka utaratibu wa viti maalum kwa wanawake kuwa asilimia 15 ya viti vyote vya wabunge ambako kulifanyika ili kutambua hayo kikatiba. Sambamba na hiyo, pia mwaka huo huo 1992 kulifanyika mabadiliko yenye kurekebisha taratibu za uchaguzi wa Rais wa Muungano na pia kutoa rukhsa na uwezo kikatiba wa kumuondoa Rais madarakani endapo tu Bunge litapiga kura ya kutokuwa na imani na Rais sambamba na kuanishwa nafasi ya Waziri Mkuu kikatiba.

Pia, mwaka huo huo 1992 Katiba ilifanyiwa marekebisho na kuipa Tume ya Taifa ya Uchaguzi jukumu la kusimamia chaguzi za madiwani.

Mwaka 1994, Katiba yetu ikapachikwa “kiraka” kingine ambapo ilikuwa ilifanyiwa badiliko dogo la kuwa na mgombea mwenza wa nafasi ya Urais ambaye baada ya ushindi huwa ni Makamu wa Rais.

Sambamba na badiliko hili, mwaka huo huo (1994) badiliko jingine katika katiba lilifanyika. Badiliko hili lilikuwa shubiri kwa ujenzi wa demokrasia na haki za binadamu nchini kwetu. Ibara ya 34 ya Katiba ilibadilishwa na kuzuia wagombea binafsi. Uamuzi wa jabu sana! Ambao hata marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kuupinga hadharani katika sherehe za Mei Mosi 1995 (sikukuu ya wafanyakazi). Mwalimu alimgeukia marehemu Waziri Basil Mramba na kumwambia; “Ndugu Waziri huwezi kumnyang’aya Mtanzania haki yake ya Uraia ya kuomba kuchaguliwa na wenzake bila ya kulazimika kudhaminiwa au kuwa mwanachama wa chama cha siasa. Hii ni haki ya uraia, hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuipoka haki hii”.

Licha ya jitihada toka wadau mbalimbali kama vile mwanasiasa Mchungaji Christopher Mtikila ambaye alipigania haki hii ya kikatiba ya mgombea binafsi katika vyumba vya mahakama, na wanaharakati mbalimbali bado mpaka leo Katiba yetu haijatoa fursa hii adhimu.

Kisha mwaka uliofuata tu, yaani 1995, ambapo ndio ulifanyika Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi, kukawa na hitaji jingine la badiliko na kupachikwa “kiraka” kingine; kiapo kwa rais, Makamu wake, Waziri Mkuu na Rais Zanzibar, kuapa kuulinda muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Pia kuwekwa kwa ukomo wa Rais kuwa vipindi viwili tu ulianzishwa.

Inasemekana, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, katika nafasi ya Urais uliacha funzo kubwa ambalo baadae likapelekea msukumo wa badiliko jingine la katiba ambapo mwaka 2000 “kiraka” kingine kilipachikwa katika Katiba yetu ili kumpa uwezo na ushindi katika nafasi ya Urais yule ambaye atapata kura nyingi zaidi ya wapinzani tofauti na ilivyokuwa awali ambapo Rais alipatikana kwa kupata walau asilimia 51 ya kura zote.

Sambamba na badiliko hilo, mwaka huo huo (2000) pia yalifanyika mabadiliko mengine ya katiba ambapo; Rais alipewa mamlaka ya kikatiba kuteua watu kumi kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku viti maalum vya wanawake bungeni vikiongezwa na kufikia asilimia 20.

Na mwaka 2005 Katiba yetu iliwekwa “kiraka” kingine ambapo kwa safari hii, viti maalum vya wanawake Bungeni viliongezwa kutoka asilimia 20 hadi asilimia 30.

Kama tulivyoona hapo juu historia ya katiba Tanzania mabadiliko yote ya katiba yaliyofanyika hadi sasa hayakushirikisha wananchi moja kwa moja. Hivyo ni dhahiri kuwa katiba tuliyonayo hivi sasa haikutokana na watu (umma) wa Watanzania na hivyo si Katiba ya watu (umma). Hii ni kutokana na ukweli kuwa katiba hii imetokana na mapendekezo ya kamati kuu ya chama kilichokuwa kimeshika hatamu zote za kisiasa na ambacho si kila mwananchi alikuwa mwanachama.

Lakini pia, tulijifunza katika mchakato wa Katiba mpya 2010–2014 ambapo kuanzia Tume ya Katiba ya Jaji Mstaafu Warioba na hata Bunge Maalumu la Katiba (Constituent Assembly) zilivyojitahidi kuzunguka kila kona ya nchi na kupata pia uwakilishi wa makundi mbalimbali katika jamii kuhakikisha maoni, mawazo, fikra, na maono ya kila Mtanzania yanakusanywa, kuchambuliwa, kutathminiwa na kuhakikisha yanakuwa sehemu ya uundwaji wa Katiba mpya kwa kuwemo katika zao la Rasimu zile mbili yaani; Rasimu ya Katiba ya Tume ya Katiba chini ya Jaji Mstaafu Warioba na Rasimu ya Katiba ya Bunge Maalumu la Katiba chini ya Hayati Samuel Sitta (Katiba Inayopendekezwa).

Hatua ambayo ilikwishafikiwa katika kuwashirikisha wananchi si ya kubezwa pia ni ya kuthaminiwa kwani uwekezaji ambao ulikwisha fanyika mathalani katika muda, watu, rasilimali fedha ambazo ni kodi zetu sisi wananchi; ndiyo:- mimi na wewe si za kubezwa na kutelekezwa kirahisi.

Pia lazima tukubaliane kama taifa kuwa baada ya mchakato wote na uzoefu (historia) Katiba yetu imepitia mabadiliko ya “kupachikwa viraka” ambayo bado yanaonekana kutokukidhi matakwa ya wananchi. Hivyo basi sasa lazima tuseme imetosha na kuhakikisha tunapata Katiba mpya nzuri na bora inayotokana na wananchi wenyewe ambayo itasaidia kuwa mwongozo mpya mkuu katika uendeshwaji wa nchi yetu.

--

--

Michael Dalali

"Truth is an inseparable companion of justice and mercy"-@pontifex| Cogito Ergo Sum| Analyst| Strategist| Facilitator| Translator| Writer & Avid Reader! 🥋