Msitu wa Pugu Kazimzumbwi: Mapafu ya Dar!

Michael Dalali
8 min readNov 22, 2021

Je, umeshawahi kusikia au kutembelea msitu wa hifadhi ya taifa wa Pugu Kazimzumbwi?

Hili ni eneo la utalii lililopo nje kidogo mwa jiji la Dar es Salaam, katika mkoa wa Pwani. Ni umbali wa kama kilometa 24 hivi kutoka Posta.

Jina la hifadhi hii ya Pugu Kazimzumbwi linatokana na muungano wa misitu miwili yaani msitu wa Pugu na msitu wa Kazimzumbwi.

Msitu huu wa hifadhi unapendezeshwa na vitu vingi hasa kama wewe ni mpenzi wa mazingira, kupanda milima, miti, uoto asilia, ndege, wanyama wadogo wadogo, mpenda kupiga picha. Kwa kweli ukienda hutakosa cha kufanya na utashangazwa na uzuri uliyopo pale.

Kihistoria, msitu wa Pugu Kazimzumbwi ulipewa hadhi ya hifadhi toka mwaka 1947 na kisha mnamo mwaka 2020 ulipanda hadhi na kuwa msitu wa mazingira asilia. Hapo zamani, msitu huu uliitwa ‘Msitu wa Mogo’ yaani ‘Nyundo’ jina lenye asili ya Kigiriki na Kilatini. Jina hili lilibadilishwa baada ya uhuru na kua ‘Pugu Kazimzumbwi’.

Katika kipindi chote hiki, huu msitu haujawahi kupata umaarufu wa kutosha. Na labda kwa sababu ni wachache kati yetu ambao tunafatilia kwa ukaribu au kuchukua muda na kufanya utalii wa ndani, na hivyo kuweza kuujua msitu huu hasa ukiacha wale ambao wanafanya kazi za tafiti zinazohusisha misitu.

Heko kwake Mheshimiwa Jokate Mwegelo ambaye amekuwa kinara kwa kuutambulisha na kuutangaza msitu huu hasa kupitia jitihada zake mathalani tamasha lake la Ushoroba. Kwani kati ya mwaka 2018 na mwaka 2021, Mhe. Mwegelo alikuwa ndiye Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe. Katika kipindi hiki hakika atasifiwa kwa kuweza kuitangaza na kuinyanyua Wilaya ya Kisarawe kuwa kati ya wilaya bora ikiwa ni pamoja na kutangaza fursa mbalimbali zilizopo katika wilaya hii. Na ni katika hiki kipindi aliweza kuutambulisha kuupa mashiko msitu wa hifadhi wa Pugu Kazimzumbwi.

Ushoroba neno la Kiswahili likiwa na maana ya njia au lango, ambapo kwa matumizi ya neno/jina hilo lilikuwa na lengo hasa kwamba Kisarawe ni lango au njia mpya kuelekea katika vivutio na maeneo yenye fursa ambazo hayakuwa yakitambuliwa awali ikiwemo pia kutambua njia hiyo na vivutio vyake kuelekea katika mbuga kubwa Afrika, Selous Game Reserve yenye ukubwa wa takribani kilomita za mraba 54,600 na kwa mwaka 2020 ikabadilishwa jina na Rais wa awamu ya tano, John Pombe Magufuli na kuitwa; Nyerere National Park.

Kihistoria, msitu wa Pugu Kazimzumbwi ulipewa hadhi ya hifadhi toka mwaka 1947 na kisha mnamo mwaka 2020 ulipanda hadhi na kuwa msitu wa mazingira asilia. Pia ifahamike, zamani jina la msitu lilikuwa msitu wa Mogo lenye maana ya nyundo. Mogo ni neno lenye asili ya Kigiriki na Kilatini. Baada ya Uhuru, jina hili la Mogo likabadilishwa na kupewa sasa majina ya misitu ya sasa yaani msitu wa Pugu na Msitu wa Kazimzumbwi.

Moja kati ya vitu vinavyotofautisha msitu huu na misitu mingine ni Panzi aliyepambwa kwa rangi za bendera ya Taifa (yaani bluu, njano, nyeusi, na kijani). Panzi huyu ni maarufu kwa jina la Ushoroba au kwa jina la kitalaamu ‘Cyphocerastis Uruguruensis’. Inasemekana kuwa msitu wa Uruguru, Morogoro nayo ina panzi wa aina hii ila tofauti yake ni mpangilio tu wa rangi hizo.

Hakika Panzi Ushoroba hupendeza mno hasa anapokua apaa na kuruka juani. Uzuri wa rangi zake ni kivutio tosha cha kukufanya ustaajabu hata kwa dakika moja!

Inategemea uko katika wakati gani na unapenda kufanya nini, Msitu wa Pugu Kazimzumbwi una vitu vingi vya kufanya;

Kwanza kabisa kuna shughuli ya uvuvi katika bwawa linalopatikana katika msitu huu ambalo ndilo lina alama ya neno USHOROBA. Eneo hili ni maarufu sana kwa uzuri wake. Mgeni hutumia ngazi ambayo ipo ili kufika ndani kidogo ya bwana na kuweza kupata mandhari ya kupiga picha bwawani. Watalii wengi wanaotembelea eneo hili hupenda kupiga picha katika eneo hilo kutokana na mandhari nzuri na ya kuvutia.

Bwawa hili limekuwa likitumika kama tegemeo kwa wakazi wote jirani na eneo hili la msitu, shule ya Sekondari ya Minaki na viunga vya jirani kwa kipindi kirefu. Kati ya mwaka 2018 mpaka 2019 ndipo eneo hili likaunganishwa na mfumo wa maji safi wa DAWASA na kufanya bwawa hilo kutokuendelea kuwa chanzo kikuu cha maji kwa wakazi hawa.

Bwawa hili, linahifadhi samaki aina ya perege na kambale ambapo imetoa fursa kufanyika michezo ya kuvua samaki na kuwarejesha kwenye maji. Kwa wanaopenda baada ya kuwavua, wanaweza kupikiwa na wakaweza kula pale pale. Hairuhusiwi tu kuvua na kuondoka nao.

Unapokuwa ukiendelea na utalii katika bwawa hili, unaweza pia kuendesha mtumbwi ndani ya bwawa. Mchezo huu unakupa uwezo wa kulizunguka bwawa zima na kuliona katika mawanda tofauti tofauti na mapana zaidi sambamba na kuendelea kufurahia mandhari ya msitu. Kwa kweli zoezi hili ni la kuburudisha na kupumzisha akili sana.

Unaweza ukawa unajiuliza juu ya usalama wako uwapo katika zoezi la kuendesha mtumbi, basi ondoa shaka kabisa kwani usalama ni kitu kinachozingatiwa na kupewa uzito mkubwa. Kwani katika mchezo huu na mingineyo yote, kuna mhusika ambaye anaratibu zoezi zima huku wageni wakipewa maboya ya kujiokoa kama tahadhari na kuhakikisha usalama muda wote.

Wakati ukiendelea kufurahia mazingira ya eneo hili, unaweza kushuhudia sehemu ya msitu yenye kusheheni miti aina ya mianzi (bamboo) ambayo iko pembeni kidogo mwa bwawa. Cha kushangaza ni kwamba, mianzi hii ina miiba na inasemekana kuwa, lengo kuu la kupanda mianzi hii mnamo mwaka 1977 ilikuwa kuzuia mmong’onyoko wa udongo kwa kipindi kile.

Eneo hilo ni tulivu sana na lina kivuli chenye ubaridi kinachokuwepo muda wote wa siku kwani mianzi imefunga vizuri na kuruhusu kwa uchache sana mwangaza wa miale ya jua kupenya. Utulivu huo, ni kivutio cha kipekee kwa wenye kutaka kufanya camping; kujitenga na dunia kufanya mafungo au sala (retreat) au kutafakari (meditation).

Pia kwa utulivu uliopo katika msitu huu, yapo maeneo maalumu ambayo hutumiwa kufanya yoga. Na utulivu wake hupendwa sana na wenye kupenda yoga.

Ifahamike, msitu huu unaweza kutembelewa na watu wa kila aina na rika, maana una shughuli nyingi za kumfaa kila aina ya mtu na rika lake. Kuna wenye kuutembelea na kufanya mazoezi kwa kukimbia, wapo ambao wanafanya mazoezi kwa kutembea na kupanda vilima. Lakini pia wapo watu wanaokuja kwa ajili ya mapumziko tu, kupata mlo na kufurahia mazingira.

Msitu huu hutumiwa pia kufanya mazoezi na maandalizi hasa kwa wale ambao wanataraji kupanda milima mirefu kama Mlima Kilimanjaro. Kuna njia mbalimbali za kuuandaa mwili na za umbali tofauti.

Kupanda kilima ni shughuli nyingine unayoweza kufanya hapa. Kuna kilima chenye urefu wa 277m juu ya usawa wa bahari. Kilele cha kilima hiki ni maarufu kwa jina la Msolo. Ili kufika kileleni itakubidi kupanda vilima takribani saba (7) ambavyo ni tofauti tofauti. Na katika safari ya kupanda kilima hiki, umakini unatakiwa maana unapoelekea kufika juu kabisa kuna mwinuko mkali ambao mara nyingi itahitajika msaada wa kutumia kamba katika kupanda.

Ukiwa unaendelea kupanda kilima hiki na ukafanikiwa kufika kwenye kilele Solo, kadiri ya hali ya hewa ya siku hiyo unaweza ukabahatika kuona vyema jiji zima la Dar Es Salaam.

Jina la kilele hiki limetokana mti asili ‘Msolo’ ambao kwa kipindi cha miaka mingi umekuwa ukitoa matunda/mbegu zijulikanazo kama solo ambazo hutumika katika kucheza mchezo wa bao.

Solo

Safari ya kushuka toka kilele cha Solo hutumia njia nyingine tofauti na ambayo umeipandia, hii inaendelea kukupitisha katika mandhari mazuri ya msitu wa Pugu Kazimzumbwi, ikiwemo kuona vizuri bwawa kutokea juu ya kilele ambapo huvutia sana.

Pia utapita mahala ambako kuna pango ambalo matambiko ya asili ya wakazi wazawa huwa wanafanya kuomba mizimu. Shughuli hizo za matambiko zingali zinaendelea mpaka sasa kadiri ya ratiba na taratibu maalumu zilizowekwa na mamlaka ya msitu.

Inasemekana mzimu uliopo katika msitu wa Pugu Kazimzumbwi ni Mzimu wa Mavoga. Mzimu huu una simulizi mbalimbali za kusisimua ambazo zinastahili makala yake pekee ya kutosha kuzibeba.

Eneo hilo la matambiko ni eneo pia linaloaminiwa kama chanzo au kitovu asili cha uwepo wa bwawa la maji na nyakati za mvua basi eneo hilo huwa na maanguko ya maji (waterfalls) yenye kutoa taswira nzuri ya kuvutia. Ni eneo lenye kudumu katika ukimya na lisilohitaji kelele.

Ukiwa unashuka kuelekea chini, utajikuta upo tena pale Bwawani ambako ndiko ulipoanzia mwanzo. Muda huu utagundua uzuri wa aina mbalimbali ya miti. Niliangalia kuanzia chini mpaka kwenda juu nikistaajabu.

Msitu huu umesheheni miti aina ya “Mipugu” ambayo ndiyo hasa imebeba jina la Pugu. Miti hii ipo kwa mtindo wa Kamba Kamba zinapinda na kujiviringisha juu ya miti mingine. Na ipo mipugu mingine ambayo inasimama yenyewe inategemea na aina na umri wake.

Aina mbalimbali za miti ya mipugu

Pia utakutana na miti mingine inaitwa “Minaki’ sawa na jina la shule Sekondari maarufu yaani Minaki Sekondari.

Muonekano wa Mipugu ni miti ambayo imekaa kama kamba kamba zinazojifunga aidha zenyewe au nyakati zingine juu ya miti mingine. Jina la miti hii ndiyo chimbuko la jina la Pugu eneo na pia shule ya Sekondari ya Pugu iliyopo kilomita chache kabla ya kufika eneo la msitu. Hakina eneo hili ni la kihistoria hasa tukimkumbuka Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alipata kufundisha shule hiyo kabla ya kuacha na kutumikia siasa za kusaka uhuru wa Tanganyika.

Ukiacha miti asili ya Mipugu na Minaki, msitu huu pia umesheheni miti asili ya aina kwa aina, sambamba na maua mazuri sana ambayo yako ndani ya msitu. Vilevile kuna wanyama ambao ni vivutio vya utalii kama; Mbega weupe na Mbega weusi, Digidigi, Nguruwe pori, Nungu nungu, Komba, Ngedere, Kima, Nyani, Mijusi ya aina mbalimbali, Nyoka wa aina mbalimbali, Vinyonga, Siafu (Red ant) na Sungusungu (Black ant). Msitu huu pia umepambwa na aina mbalimbali za ndege ambao huja na kuondoka kadiri ya nyakati sauti na milio yao huburidisha ajabu.

Pamoja na juhudi za kuulinda huu msitu ili kuendelea kuhifadhi uzuri wake kwa vizazi vijavyo, bado unakumbana na changamoto mbalimbali hasa shughuli za kibinadamu kinyume na sheria mathalani wananchi ambao wanavamia eneo la msitu na kukata kuni au miti kwa matumizi mbalimbali.

Pia kumekuwa na changamoto ya miaka mingi ambapo wananchi jirani kuvamia eneo la msitu na kuanza kuchochea kusogezwa kwa mpaka wa msitu huu ikiwa kwa kutumia mbinu kama kulima eneo la msitu au hata kuchoma moto. Vitendo hivi vinarudisha nyuma sana uhifadhi wa msitu huu ambao umekua tunu hasa katika kuhakikisha hewa safi kwa jiji la Dar Es Salaam.

Mbali na changamoto zilizopo, msitu huu umekuwa na faida nyingi ikiwemo kuzalisha asali tiba yaani asali chungu ambayo imekua ikitoka katika mizinga ya nyuki iliyoitegwa kwenye baadhi ya maeneo ya msitu huu. Asali hii hutumika kwa matumizi ya binadamu.

Faida nyingine ni kuwa chanzo cha ajira na shughuli za kiuchumi ambazo zinanufaisha sana vijana wanaouzunguka msitu lakini pia hata ambao wapo nje ya mazingira ya msitu kwa kuongoza shughuli mbalimbali za utalii na kutoa huduma mbalimbali kwa watalii wanaofika msituni.

Misitu ni uhai na ina faida lukuki katika uhai na utulivu wa maisha yetu kwa ujumla. Ninawahamasisha wote kuutembelea msitu huu na mingine yote hapa nchini. Sambamba na kuitembelea, pia shime tushiriki kuilinda, kuijali na kuipenda misitu yetu hii kwa manufaa ya vizazi vyetu vya sasa, baadae!

--

--

Michael Dalali

"Truth is an inseparable companion of justice and mercy"-@pontifex| Cogito Ergo Sum| Analyst| Strategist| Facilitator| Translator| Writer & Avid Reader! 🥋