“Mwana; tazama Mama yako”!

Michael Dalali
4 min readOct 24, 2022

Bwana wetu Yesu Kristu, katika wakati wake wa mwisho hapa duniani akiwa juu ya msalaba pale Golgota — kabla ya kuuacha ulimwengu alihakikisha anatukabidhi katika mikono salama; kwa kinywa chake alitupa Mama Bikira Maria; Mwana, tazama Mama yako. Kisha pia alimkabidhi Mama sisi wanae; Mama, tazama mwanao (Rejea Yohane 19: 26–27).

Kwa maneno mengine kadiri ya tamaduni zetu za kibantu, Yesu alitupa wosia kabla ya kufa kwake na kutuweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Mama Bikira Maria.

Ni kama vile tu ambavyo katika familia zetu pale ambapo Baba au Mama wa familia anapokuwa karibu na umauti na kuwaita watoto, wanafamilia au wanaukoo kisha kutoa maagizo ya mwisho. Daima huwa tunayaheshimu na kuyaishi. Daima tunawaheshimu na kuwakimbilia kupata ushauri au kuwashirikisha masuala mbalimbali wale ambao tunakuwa tumekabidhiwa kwao kama wasimamizi wetu kifamilia au ukoo.

Katika muktadha huo, Mama Bikira Maria anapashwa kukimbiliwa daima na kila mkristu. Anapashwa kuwa karibu sana kwa kila anayemuamini Yesu Kristu. Ndiye Mama ambaye yu kwa ajili yetu. Tunapashwa kuzungumza nae kila saa kwa kupitia sala na tafakari zetu.

Wakati wa mahangaiko na kutanga tanga katika dhiki, shida na changamoto za kimaisha; Mama huyu anapashwa kuwa kimbilio letu. Mama huyu anapashwa kuwa mfariji wetu. Daima mikono yake iwazi kutupokea na kutukumbatia. Yeye ni mlinzi wetu mithili ya kuku alindavyo vifaranga vyake dhidi ya mashambulizi mbalimbali iwe mwewe au nyoka au kito chochote hatari. Lakini kama ambavyo Mtetea anakimbilia vifaranga vyake; vivyo hivyo vifaranga huwa daima vionapo hatari hukimbilia kujificha chini ya mbawa za Mama yao. Nasi tunapashwa kukimbilia ulinzi wa Mama Bikira Maria, tunapashwa kujikinga na kujificha chini ya mbawa zake — hapo ndipo tutakuwa salama daima.

Tunaalikwa daima kusali rozari pamoja na sala nyingine nyingi za kutuleta karibu na Mama Bikira Maria. Rozari inapashwa iwe sehemu ya maisha yetu hata zaidi ya miezi iliyochaguliwa na kutengwa maalumu na Kanisa kama miezi ya kusali rozari yaani mwezi Mei na Oktoba.

Maombezi ya Mama huyu daima yamethibitika kuwa na matokeo bora hata katika nyakati ambazo labda bado muda muafaka wa kupata suluhu lakini pundi Mama Bikira Maria anapoingilia kati na kushiriki maombezi hayo; matokeo huwa mazuri.

Mwinjili Yohane (rejea Yohane 2: 3–10) anatukumbusha kisa cha Mama Bikira Maria na Yesu Kristu pale ambapo Mama Bikira Maria alipomfata kumlilia shida lakini Yesu aliona ule haukuwa wakati sahihi wa kuanza kujidhihirisha kupitia miujiza lakini kwa neno la Mama; alitenda. Muujiza maarufu wa Kana ambapo Yesu alibadili maji na kuwa divai. Mama Maria baada ya kuona mambo yameshaharibika katika tafrija ile kwa kukosekana divai ya kutosha aliokoa jahazi kwa kumfata mwanae; “Hawana divai”. Lakini jibu ambalo labda Mama hakutaraji kwa mwanae, Yesu alimwambia; “Mama, usiniambie la kufanya. Saa yangu bado”. Tunajifunza licha ya ukakasi wa jibu hili kwa jicho la kibinadamu na makuzi — mahusiano baina ya Mama na Mwana; Mama aliweka imani kuu kwamba Mwanae, Bwana wetu Yesu Kristu hawezi kuacha ombi lake na ndiyo maana licha ya jibu hilo aliwaambia watumishi; “lolote atakalowaambieni fanyeni”!

Mapenzi ya Mama kwa mtoto wake daima hayaelezeki na vivyo hivyo amani na utulivu ambao mtoto anakuwa nao akiwa kwa Mama yake hauelezeki; basi ndivyo ambavyo tunapashwa kujisikia huru na kuzungumza na Mama Maria kupitia sala za maombezi yake.

Kwa upande mwingine; mwaliko wa Yesu kwetu sisi (mwana) kumtazama Mama Bikira Maria — tunapewa fursa ya kufuasa maisha ya Mama Bikira Maria. Maisha ambayo yamejaa imani kuu, maisha ambayo yanamruhusu MUNGU kuyaongoza — FIAT!; “mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyonena! (Luka 1: 38)”

Kwa maisha ya Mama huyu, yapo mengi (hata makala hii haitoshi kuyaeleza) ambayo tunapashwa kuchota na kujifunza katika maisha yetu mathalani unyeyekevu wake, kustahimili machungu na mateso makali, na daima kubaki imara na thabiti katika kumtegemea Mungu. Hebu fikiri alikuwa bega kwa bega na mwanae katika mateso, kifo msalabani hadi kumlaza kaburini; ni uchungu wa namna gani?!

Kristu anapotuambia; tazama Mama yako — ni pamoja na yote haya, yaani kumwangalia yeye na mienendo yake kama mfano na kioo kwetu katika maisha yetu.

Hapa ni uhakikisho tosha kwamba tukimwelekea Mama huyu katika sala na maombezi kupitia kwake, hakika hatotutelekeza haijalishi udhambi wetu au upo katika mahangaiko gani. Atakuwa nasi bega kwa bega daima. Na ndiyo maneno mazito yaliyopo katika sala ya Kumbuka yakidhihirisha haya; “Kumbuka, Ee Bikira Maria mpole sana, haijasikilika kamwe kwamba ulimwacha mtu aliyekimbilia ulinzi wako, aliyeomba msaada na maombezi yako…..!”. Basi nasi daima tumkimbilie Mama yetu mpendwa huyu. Tuwe nae siku zote muda wote.

Tumsifu Yesu Kristu!

--

--

Michael Dalali

"Truth is an inseparable companion of justice and mercy"-@pontifex| Cogito Ergo Sum| Analyst| Strategist| Facilitator| Translator| Writer & Avid Reader! 🥋