Michael Dalali
10 min readOct 15, 2018

--

Taifa la watawaliwa kuliko raia; rahisi kuangamia!

Taifa lolote ili listawi, lina mengi hasa namna gani linawekeza katika watu wake kwa kuwapa elimu bora, kuhakikisha afya zao zinakuwa imara, ili waweze kutumia vyema rasimali kama ardhi na bahari, ziwa na mito katika kujineemesha na kuistawisha nchi.

Kuna umuhimu mkubwa katika yote kuaangalia namna gani rasilimali watu inajengwa na kuimarishwa kama mtaji mkuu wa kwanza wa uhai wa taifa. Hapa tunaona namna gani unaweza kuwa na watu ambao wasomi wa sayansi ya siasa wameweza kuwatenga katika makundi mawili (na zaidi ila leo tuangalie haya); yaani kundi la kwanza ambalo wanawaita ‘wananchi/raia (citizens)’ huku kundi jingine likiwa watawaliwa (subjects)’.

Tafsiri rahisi ya dhana hii kadiri watawaliwa hawana la kusema juu ya watalawa wao na haki zo za msingi zimepuuzwa.Mara nyingi sababu ya kuaminishwa ya kuwa wao ni mbumbumbu wasiojua lolote juu ya msauala ya kiuchumi na kisiasa hata kama yanawagusa mojamoja. Raiakwenye tawala za kidemokrasia wanakuwa na haki ya kusaili maisha yao ya kiuchumi na kisiasa matokeo yake hupata uwezo mpana wa ufahamu na uelewa wa masuala ya nchi yake na pia kwa uelewa huo anaweza kusimamia na kudai haki zake toka kwa viongozi au watawala.

Raia hawashuki toka mbinguni bali kuna mazingira wezeshi yanayopaswa kuwekwa ili kustawisha uwezo wao wakufuatilia na kuhoji mambo ya msingi katika taifa lao.Mazingira hayo yawe pamoja na watu wa nchi hiyo kuwa na kiu binafsi na mazingira rafiki ya kusoma na kupatikana ripoti muhimu zinazoeleza kinagaubaga masuala na mustakabali wa taifa letu.

Tafakuri hii ambayo imezaa makala ni baada ya mazungumzo yaliyofanywa katika kuadhimisha miaka 60 ya shirika la kiliberali toka Ujerumani; Friedrich Naumann Foundation ambayo yaliongozwa na msomi nguli hapa Tanzania kwenye nyanja ya sayansi ya siasa, Profesa Mwesiga Baregu.

Katika moja ya sehemu za mazungumzo yake, alitanabaisha kwamba mnamo mwaka 1994 wakati wanaanzisha taasisi ya tafiti na elimu ya demokrasia nchini Tanzania almaarufu kama REDET walibaini katika moja ya utafiti ambao waliufanya kipindi hicho kwamba kama taifa tulikuwa na watawaliwa wengi (subjects) kuliko raia (citizens).

Lakini jambo jingine muhimu pia katika mazungumzo hayo; ni kubaini kwake kwamba katika hadhira ile ambayo kwa kiwango kikubwa ilikuwa ya vijana kwa kiasi kikubwa hawakuwa wamewahi kusoma ripoti ya Nyalali ya mwaka 1992. Hili lilimshtua na kumuumiza sana msomi huyo.

Kwangu hili lilinitafakarisha zaidi na kwa makala hii nashirikisha tafakari hii pana kwa taifa kwa minajili ya kuangalia namna bora ya kunusuru taifa letu hasa kwa vizazi vya sasa na baadae.

Kushtuka na kuumia huku endapo tukizunguka kwa sasa na kuuliza si tu vijana bali hata watu wazima, si ajabu tutaambulia wachache sana ambao wanaufahamu mzuri wa nini kimo na kilielezwa kwa kina sambamba na mapendekezo yale muhimu yaliyotolewa na tume ile ya Jaji Nyalali.

Kwa haraka, hiyo ni picha halisi ambayo inasadifu hali ya jamii yetu na kutokuwa na utamaduni na mapenzi ya kusaka maarifa ambayo yamo kwenye vitabu, majarida na mitandaoni. Jamii ambayo haisomi wala kuandika (ukiacha tu udaku; ambako huku naamini tu mstari wa mbele).

Hili linahitaji kuangalia kwa picha pana zaidi ambayo inaathiri taifa mathalani ni kwa kiasi gani ripoti muhimu kama hizi za tume mbalimbali zinaweza kupatikana kwa urahisi kwa kila mwananchi anapozihitaji wakati wowote. Sehemu kubwa ya nyaraka hizi za ripoti zimebaki kuwa siri kwani si rahisi kupatikana. Hivyo itafika nyakati ambapo kizazi ambacho kilikuwapo katika hizo tume au kipindi hizo tume zinaundwa kikaondoka na maarifa yake bila kurithisha taifa.

Ukiacha upatikanaji wa nyaraka hizi na ufahamu wake kwa jamii nzima, tunashuhudia pia kupuuzwa kwa makusudi utekelezwaji wa mapendekezo mbalimbali ambayo huwa yanatolewa katika tume hizi. Jambo ambalo huacha athari hasi kumea mizizi. Lakini pia kwa baadhi ya masuala; tunashuhudia kila uchao kurudia kazi ile ile upya au inayoshabihiana na ile na hasa kutokana na kutojifunza na kuweka katika vitendo somo tunalolipata kutokana na tume hizi. Tuchukue mfano mathalani Tume ya Jaji Kisanga ambayo iliundwa kuchunguza kwa kina chanzo hasa cha ajali ya meli ya Bukoba mnamo mwaka 1996. Ni kwa namna gani mapendekezo yake yamekuwa yakiishi katika mioyo ya watu na hasa wenye dhamana katika usafirishaji wa vyombo vya majini?

Tukiangalia Tume ya Nyalali, baadhi ya masuala na mapendekezo ambayo yalitolewa kipindi kile yaani mwaka 1992 yamekuwa yakiendelea kuligharimu taifa mpaka leo. Na bado tunaendelea kukwepesha na kujizungusha kutokushughulikia na chanzo na mizizi hasa ya baadhi ya changamoto zinazokabili taifa letu hasa kwenye siasa na zaidi namna ya kuiendesha siasa yenyewe tukihakikisha tunakuwa na siasa safi kama mtaji muhimu wa kuchochea maendeleo.

Tunapaswa kufahamu hasa raia kwamba uundwaji na ufanyaji kazi wa tume mbalimbali huligharimu fedha nyingi sana taifa letu. Hivyo kazi zake na mapendekezo yake yanapaswa kuwa msingi imara wa kuvusha taifa toka hatua moja kwenda nyingine na sio tu kuonekana kufanya jambo huku dhamira ya dhati kuliishi hakuna, yaani inakuwa kiingereza wanasema; tick a box.

Jukumu hili la kuelimisha ambalo hivi sasa tunashuhudia kuwa limebaki zaidi katika kujikita kwenye elimu ya mpiga kura kuliko utoaji wa elimu ya uraia ambayo inapaswa iwe kila uchao ni jukumu pana sana na lenye kuleta wadau wote katika jamii kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.

Ni namna gani kama mzazi unahakikisha mtoto au kijana anakuwa na ufahamu mpana wa sheria za nchi, haki na wajibu wake katika jamii.

Hapa nakumbuka kisa kimoja kilichotokea Mei 11, 2008 katika ukumbi wa Diamond Jubilee ambapo Mzee Edrissa Mavura kwenye harusi ya kijana wake, Togolani Mavura alimpatia vitabu viwili na kumsisitiza awe makini kuvisoma na kuviishi. Wengi tumezoea wazazi kuwapa vitabu vya dini mathalani Biblia au Quran kama nguzo imara ya kiroho ambayo itaongoza maisha ya kijana hata kwenye mambo yasiyo ya kiroho baada ya kuchota maarifa yake. Lakini Mzee Mavura ukiacha Quran aliyompatia kijana wake, alimpa pia Sheria ya Ndoa ya 1971 na katika mazungumzo yake alifafanua kwamba alikwisha wahi kumueleza na kumpatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo ilimuwezesha kufahamu vyema mipaka na haki, sasa kwasababu alikuwa anaingia katika maisha ya ndoa basi alimkabidhi sheria ya nchi kwenye suala la ndoa. Hii ilikuwa naamini ishara na kilele cha namna gani pia mzazi anaweza kuwa chachu na mchango mkubwa na muhimu sana kuhakikisha taifa linakuwa na raia makini.

Taifa kwa ngazi zote na wadau wote, ni namna gani wanashiriki kwa mapana hasa kuhakikisha kundi kubwa la vijana (na watoto) ambalo ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu nchini inakuwa na maarifa mapana ya elimu ya uraia.

Ukitafakari kwa kina, kijana ambaye amezaliwa mwaka 2000 sasa ni kijana mwenye umri wa kikatiba wa kuweza kufanya maamuzi kama kumchagua kiongozi au hata naye kuchaguliwa (ukiacha tu nafasi ya Urais ambayo inamhitaji mtu mwenye umri kuanzia miaka 40 na kuendelea).

Kwa kuzingatia baadhi ya matukio kama nchi kufanya maamuzi ya kuingia katika mfumo wa vyama vingi (1992), Azimio la Arusha (1967), Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi baada ya kurejea katika mfumo wa vyama vingi (1995), mazingira ya kuanzishwa kwa vyama vingi, asasi nyingi za kiraia, vyombo vya habari binafsi kwenye miaka ya 1992 na kuendelea; haya baadhi wameyashuhudia kwa macho na kuona na kuelimika kutokana nayo na baadhi wanaona kawaida (take for granted) na kudhani uelewa ule pia unaweza ukawa katika kundi jipya hili la vijana ambao kwa sasa nao wameshapevuka na kuingia katika umri wa kufanya maamuzi ya nchi. Maswali ya msingi sana; Wanaandaliwa namna gani? Nini tunawapa? Tunaweka mifumo gani nje ya ile ya elimu ya darasani kuhakikisha wanapata elimu ya uraia muhimu kwa wao kuwa raia makini?

Kizazi hiki sasa cha vijana ambacho kwa baadhi hawana ufahamu mpana wa masuala hususan ya kisiasa na historia ya nchi yao wanashika nyadhifa mbalimbali katika sekta kama za uchumi, siasa, burudani nk. Hawa baadhi wanaweza kuwa na changamoto nyingi za kiuongozi ambazo zingeweza kuepukwa. Hili linaenda sambamba na namna gani kama taifa tunapika viongozi wetu kwenye nyanja mbalimbali ili kusudi tupate viongozi bora na imara na si kuachia kudra za Mwenyezi Mungu au kufanya kama mchezo wa bahati nasibu; kwamba unaweza kubahatika kupata kiongozi bora na unaweza pia kuangukia kwenye mikono mibovu sana. Lakini kwa elimu pana na hata historia inaweza kuwa taa na nguzo makini kwao kwa kuwapa tahadhari ya namna bora wao waenende, nani , taasisi gani, au nchi gani wawe nazo makini wakati wakihusiana nk

Baadhi ya vijana (hata wenye umri zaidi ya ujana yaani zaidi ya miaka 35) wamekuwa wakifahamu baadhi ya mambo ya nchi (kama maudhui ya ripoti mbalimbali kama Nyalali, Katiba, masuala ya Muungano, Dira ya Maendeleo ya 2025 nk) ni kama bahati tu! Sio kwamba ni zao la uwepo wa mfumo maalumu na yenye uimara ambao unafatwa kuhakikisha kila mmoja anapata maarifa na ufahamu.

Mathalani kuna baadhi ya wanafunzi wa wahadhiri au walimu ambao walipata neema kupita mikononi mwa walimu, wahadhiri ambao walikuwa wanaelimisha vyema na kuwaandaa vijana zaidi ya hitaji la kimtaala mfano hai ni Mhadhiri kama Hayati Prof. Haroub Othman pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mara kwa mara aliweza kushibisha na kufungua bongo za wanafunzi wake hata katika mambo mengi sana nje ya kile ambacho Chuo kilimtaka afundishe lakini kwake aliona wanafunzi wake wanapaswa kufahamu kwa mapana na marefu. Nakumbuka namna ambavyo alitueleza kwa kina nini hasa mantiki ya uamuzi wa nchi kuingia katika mfumo wa vyama vingi mnamo mwaka 1992 kwani yeye (Prof. Haroub Othman) alikuwa mmoja wa wajumbe wa Tume ya Nyalali. Na ilikuwa raha iliyoje kupata maarifa haya kwa watu wenyewe ambao ndiyo walizunguka nchi nzima na kuwa sehemu ya kazi ile.

Prof. Haroub alituelimisha kwamba haikuwa tu huruma ya kuona wale wachache ambao ndiyo walisema wanataka nchi iwe na mfumo wa vyama vingi kuwapa kadiri ya maamuzi yao bali katika kusikiliza hoja ambazo zilitolewa na wale ambao walipendekeza nchi ibaki katika mfumo wa chama kimoja walibaini mapendekezo ambayo walitoa ya namna mfumo wa chama kimoja uboreshwe ilikuwa ni lugha nyingine yenye kuhitaji tu mfumo wa vyama vingi. Hivyo ndivyo busara ikawaongoza kwamba ni kheri nchi ikaingia katika mfumo wa vyama vingi.

Na maarifa haya, Hayati Prof. Haroub aliweza kutoa katika nyanja nyingi sana ambazo alipata ujuzi, maarifa kuweza kurithisha wengine hasa wale ambao wamepita kwenye mikono yake na pia kwa kutumia maandiko yake na michango yake kwenye majukwaa mbalimbali.

Natambua hofu ambayo baadhi ya viongozi au tuwaite watawala wanaweza kuwa nayo dhidi ya kuwa na jamii iliyoelimika, yenye kufahamu vyema haki na wajibu wao kwamba jamii hii itakuwa ngumu sana kuitawala. Je, hofu hii ina mashiko? Ina ukweli kiasi gani? Ni jambo bora sana kulisoma zaidi na kulitafiti.

Lakini pia, tunaweza kwenda mbali na kuangalia gharama ambazo taifa lenye lindi la ujinga na lenye wananchi ambao hawajui haki, wajibu na stahiki zao kama raia linapata.

Ndiyo maana hata baadhi ya taasisi za tafiti zinafanya tafiti na katika baadhi ya mambo wanaangalia na kupima kiwango cha elimu na mwenendo wa maamuzi ya kisiasa wanayofanya mathalani ni kwa kiasi gani chama fulani kinapendwa au kuchaguliwa na kundi la watu wenye elimu isiyozidi shule ya msingi na kwanini chama fulani kinapendwa na kuchaguliwa na kundi la watu wenye elimu kuanzia shule ya msingi na kuendelea au chama fulani kinachaguliwa na kupendwa zaidi na watu wenye elimu ya juu. Tunaweza kuona mfano hapa nchini, taasisi kama Twaweza kupitia mradi wake wa Sauti za wananchi aina ya maswali na majibu yake kadiri ya makundi, umri, kiwango cha elimu nk.

Lakini kumnyima maarifa muhimu raia na kutokumjengea uwezo, ni faida ya muda mfupi tu kwa yule mwenye kuiangalia katika jicho la kuweza kutawala kwa amani. Kwani hata katika kutawala angalipiga hatua zaidi endapo jamii ingekuwa na uwezo mkubwa na hata ushiriki wao (ambao mara kwa mara tunatoa rai kwa jamii ishiriki mambo ya nchi) unakuwa mashakani kwani hawana ufahamu mpana. Chukua mfano hai; haikuhitaji kutumia rasilimali kubwa kama ya fedha na muda nk katika kuhamasisha jamii kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwamba kuna umuhimu wa kudai risiti endapo kila raia angalikuwa anafahamu vyema athari chanya ya kuhakikisha anadai risiti na namna gani inakuwa na uhusiano wa moja kwa moja na ustawi wake kwani kile ndicho kithibitisho cha ulipaji wa kodi toka kwa mfanyabiashara au huduma yoyote ambayo anapatiwa. Raia huyu angekuwa tayari anafahamu madawa, hospitali bora, maji nk ambazo anadai kama haki yake Serikali impatie vina uhusiano na uwezo wa Serikali katika kukusanya kodi, hivyo basi nae ana mchango wa kuhakikisha anaziba mianya yote. Tofauti na sasa, wananchi wanadai risiti ili tu asije akitembea mbele akakamatwa na afisa wa TRA ambaye atamhoji risiti ya bidhaa alizonazo. Inamaana kuna uwezekano juhudi kama hizi zisiwe endelevu kwasababu hazijawekewa mizizi toka awali.

Natambua changamoto nyingine kubwa ambayo ipo kwa sasa ukiacha utamaduni mdogo wa kujisomea pia uhaba na ugumu wa upatikanaji wa vitabu na machapisho makini. Taifa lingeweza kuwa linaelimika kwa upatikanaji rahisi na wa kutosha wa machapisho, vitabu na majarida mbalimbali ambayo yameandika kwa kina masuala ya historia ya nchi yetu, elimu ya uraia, mafunzo na uzoefu toka kwa watu ambao wamekwisha shika nyadhifa mbalimbali katika sekta mbalimbali nchini-hili bado ni tatizo kubwa ambalo tunaweza kuliweka katika viwango vya kustahili kuwa janga la taifa.

Kuna vitabu na machapisho ni muhimu sana kama taifa na yanapaswa yawe yanahakikisha yanapatikana wakati wote haijalishi yana uhai wa miaka mingapi toka yachapwe.

Kuna nyakati chapisho kama Azimio la Arusha (1967) halikuwa likipatikana kirahisi. Jambo ambalo linapelekea kizazi kipya kuwa na maarifa nusu juu ya azimio hilo au kutokuwapo kabisa na ufahamu ukiacha tu kujua jina.

Au tunaona hotuba muhimu sana kwenye taifa ambazo zilikwisha kutolewa na viongozi na kutoa mafunzo na kuweka msingi imara kwa taifa hili zilivyopotea kwa wananchi hasa kizazi baada ya viongozi hao.

Ndiyo maana tunashuhudia baadhi ya wadau kama HakiElimu walivyofanya juhudi za kuchapa Azimio la Arusha au Kigoda cha Mwalimu Nyerere na pia Kavazi la Mwalimu Nyerere wakijitahidi kuhakikisha wanachapa hotuba na machapisho ya Mwalimu Nyerere ili kuhakikisha jamii hasa kizazi kipya kinapata maarifa haya ambayo ni tunu kama taifa. Lakini pia, kuna matukio ambayo yalikwisha kutolewa ufafanuzi na elimu pana kupitia hotuba hizo; tunayashuhudia yalijirudia hiyo kwa kuwa na ufahamu mpana wa historia haiwi changamoto kujua wapi pa kuanzia.

Lakini, wapo wasomi wa masuala ya kijamii, siasa na sheria nk ambao wameandika kwa kina mambo muhimu sana ya nchi yetu-nakala za kazi zao zimebaki kwa wachache mno na wale ambao wamebahatika kurithi toka kwa wazee wao au ambao walibahatika kuwa navyo. Lakini maarifa yaliyomo katika maandiko hayo yangelipaswa kuhakikisha yanapatikana kwa urahisi kwa vizazi vyote kwa wakati wote. Hivyo ni rai kama taifa kuhakikisha baadhi ya kazi hizi nzuri na zenye tija kwa taifa ambazo zimekwisha wahi kuandikwa tunahakikisha zinachapwa upya na kuwa na mfumo wa kuhakikisha zinafika kwa wananchi.

Namna gani tunahakikisha tunakuwa na wananchi au raia makini ndivyo ambavyo taifa linaweza kustawi au kujifungulia milango kuangamia. Kila mmoja ana wajibu wa kustawisha taifa kwa kuhakikisha anakuwa chachu na sehemu ya kupata idadi kubwa ya raia na viongozi makini. Ni kwa namna gani tunaacha kasumba ya kuchukulia kwa wepesi (take for granted or ignore) masuala muhimu ya nchi hata katika mitandao ya kijamii mathalani makundi kwenye mitandao ya whatsapp au mitandao mingine hasa ukikuta mtu anapotosha ukweli au kupindisha taarifa. Kwani mabadiliko huanza na mtu mmoja mmoja katika ngazi na nyakati yoyote. Tunasimama kiasi gani kuhakikisha tunakuwa sehemu ya kujenga taifa imara na madhubuti?

--

--

Michael Dalali

"Truth is an inseparable companion of justice and mercy"-@pontifex| Cogito Ergo Sum| Analyst| Strategist| Facilitator| Translator| Writer & Avid Reader! 🥋