Michael Dalali
7 min readDec 29, 2021

--

Vitabu nilivyosoma katika mwaka 2021

Namshukuru Mungu kwa neema na baraka zake tele ndani ya mwaka mzima 2021. Tunaposubiria kuanza mwaka mpya, 2022 ni vyema kama ambavyo kwa miaka kadhaa sasa nimekuwa nashirikisha vitabu nilivyosoma na namna ambavyo vilinigusa. Ifahamike, utamaduni huu dhumuni kuu ni katika kuchochea usomaji vitabu sambamba na uandishi wa vitabu nchini mwetu Tanzania kwani maarifa na ilmu imefichwa ndani ya kurasa.

Kwa sehemu kubwa kwa mwaka huu nimejikuta nikisoma vitabu vya tawasifu na vyenye kuzunguka katika mtindo huo.

Kwa idadi nimesoma kikamilifu vitabu 16 huku orodha ikiwa haijahusisha vitabu ambacho sikumudu kumaliza na kujikuta nimeishia njiani au kuviweka pembeni kabisa.

Mwaka 2021 ulikuwa pia mwaka wa baraka katika familia yetu kwa Mke wangu, Mercy Rahma Bajun kuweza kuchapa na kuzindua rasmi kitabu chake cha The Wave: Migraineur memoir juu ya anayopitia katika ugonjwa wa Kipanda uso kikali; kwa kukosa neno sahihi la Kiswahili kubeba uzito hasa wa ugonjwa huo kwa usafaha wake kama unavyoelezwa kwa kiingereza; Migraine. Hiki nimekisoma wakati kinaandikwa, na hata katika hatua za kuelekea kuchapwa na baada ya kuchapwa. Angalau ni ahueni kushika kitabu cha mwenza na ni faraja hasa kwangu. Bila shaka kitasaidia kupunguza zogo la marafiki juu ya miswada yangu inayododa bila kumaliziwa, hahahaha!

Tawasifu nyingine ambayo ilinigusa hasa na kufungua macho kwa mengi ni juu ya maisha ya Jaji Rufani Mstaafu; Steven James Bwana ambayo ameiita; Maisha yangu, Utumishi wangu. Humu kuna mengi nimemudu kuchota hasa juu ya mifumo yetu ya utoaji/usimamiaji haki ndani ya mahakama. Nimejifunza pia haiba ya mtu mathalani upole/unyenyekevu inavyoweza kukumbana na changamoto mahala pa kazi na dhidi ya wanaomzunguka. Na zaidi, nimeguswa na maisha ya sala na kumtumainia Mungu daima.

Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimaarufu “Mzee Rukhsa” alitupa fursa kusafiri katika maisha yake kupitia tawasifu yake aliyoipa jina Mzee Rukhsa. Hakika kama alivyopata sema; maisha ni hadithi tu, tujitahidi kuacha hadithi nzuri itakayosomwa. Basi kuna mengi pia nilimudu kuchota hasa jinsi ambavyo daima ni mchaMungu. Lakini tawasifu hii bado kuna maeneo yaliacha maswali ambayo bado ningalitamani kuwapo na uchambuzi wa kina, mtazamo mwingine na hata kuhoji (critique) kama eneo la Tume ya Nyalali.

Zuhura Yunus nae alitupa fursa kumfahamu mwanamke jasiri, Biubwa A. Zahor kupitia tawasifu aliyoandika juu ya maisha yake na ushiriki wake katika mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964. Kwa tawasifu hii, Zuhura anaongeza mawanda katika historia kwa kuainisha mchango ambao hakuwa vitabuni wa wanawake katika mapinduzi na siasa za Zanzibar.

Selous, The lost Sanctity-Attilio Tagalile: kitabu hiki nilipewa na mwandishi mwenyewe ambaye ni moja ya marafiki zangu bila kujua ingalikuwa zawadi ya mwisho katika kubadilishana kwetu vitabu. Mwenyezi Mungu amjalie pumziko jema peponi. Mzee Tagalile (kama ambavyo nimezoea kumwita) ameweza kuandika kwa kina juu ya namna ambavyo maamuzi ya viongozi wetu yameharibu mazingira na upekee wa Selous ikiwa sambamba na kukatwa kwa msitu wa miti sawa na ukubwa wa jiji zima la Dar es Salaam uliopo Selous ili kupisha ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Stiegler’s Gorge (Nyerere Dam). Madhara ya kimazingira kutokana na maamuzi hayo yataendelea kuandama taifa letu kwa namna mbalimbali ya athari za kimazingira mathalani kubadilika kwa vipindi vya mvua, ongezeko la joto nk. Nathamini ujasiri wake kutumia kalamu kusimamia msimamo ambao ulikuwa unakinzana na Rais wa nchi, John Magufuli. Ni kitabu ambacho namhamasisha kila Mtanzania kukisoma.

The President’s Keepers-Jacques Pauw: ni andiko lenye kujikita kuanika maisha ya Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Jacob Zuma. Ni moja ya vitabu kwa muda nilitamani kukipata na kusoma. Kinaanika namna ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka, ushiriki wa vyombo vya usalama katika kulinda maovu huku nao wakishiriki kujitajirisha visivyo halali.

Niliyoyashuhudia Jela-Mohamed Majaliwa: mwandishi ameweza kutupa picha halisi ya hali na maisha ndani ya mahabusu zetu kwa mifano ya mahabusu Central Police sambamba na maisha ndani ya magereza kama mahabusu na wafungwa katika magereza ya Keko na Segerea. Ni simulizi ambayo inafaa kusomwa ili upate uelewa mpana wa maisha ya upande wa pili na kushiriki kadiri utakavyojaliwa iwe kwa sala, kutenda na hata kupaza sauti juu ya haja ya kuboresha magereza na mahabusu zetu ili zilinde utu na haki za binadamu. Pia kukemea ubambikiaji wa kesi kwa watu wasio na hatia.
Kama alivyosema Mohammed katika ukurasa 183 ; “Jela ni kwa ajili ya yeyote na wakati wote. Yawezekana tatizo sio wewe bali tatizo ndio likakufuata wewe aidha kwa rehema za Mungu au kwa sababu fitna za wabaya na watesi wako. Kumbe basi jifunze katika hili kuishi kama mahabusu mtarajiwa, lakini pia kuishi kwa kumuomba Mungu akuepushie mbali usikutane na maisha haya ya kuwa mahabusu au mfungwa”

Anaongeza katika ukurasa wa 182 ; “ukienda jela utakutana na watoto wadogo sawa na watoto wako uliowaacha nyumbani kwako, utakutana na wazee sawa na wazee wako uliowaacha nyumbani kwako wakilia machozi baada ya kusikia umekwenda kulala jela na mahabusu, pia utakutana na wanawake sawa na akina mama zako na dada zako au binti zako uliowaacha nyumbani kwako tena wanakutegemea kama mkuu wa familia”

In the footsteps of Mr. Kurts-Michela Wrong: ni kitabu kinachoanika maisha ya Rais wa Congo, Dikteta Mobutu Sese Seko. Mwandishi Michela anaainisha namna ambavyo Mobutu alikuwa anatawala kwa mkono wa chuma.

John Magufuli; an epitome of cowardice-Ansbert Ngurumo: ni kitabu kinachoainisha kwa mtazamo wa mwandishi nchi ilivyokuwa chini ya uongozi ambao haukuwa unazingatia haki za binadamu, uhuru wa habari nk. Mwandishi anaenda mbali zaidi kuainisha kila sura namna gani taasisi mbalimbali zilizimwa na kufungwa mdomo. Mengi ambayo yamo kitabuni yamekuwa yakilalamikiwa ndani ya mapaa ya nyumba, kwenye mazungumzo ya sirini, na baadhi kuthubutu hadharani licha ya gharama waliyolipa kwa kusema. Si mapya. Tumeyaishi. Lakini mpaka sasa, ni kitabu pekee ambacho kimeandika yale ambayo Tanzania ilipita chini ya uongozi wa awamu ya tano kwa jicho jingine la ukosoaji.

Nahusudu Falsafa, kwa mwaka 2021 nimemudu kusoma maandiko mawili ambayo yamejikita kuangalia nadharia za kifalsafa mathalani ujenzi wa hoja na namna ya kushiriki katika majadiliano sambamba na falsafa ya kistoiki (Stoicism). Argument: a guide to critical thinking cha mwandishi Perry Weddle na The Second Mountain cha mwandishi David Brooks vimechochea maarifa yangu kwa upande wa Falsafa.

Tundu Antipas Lissu aliweza kutoa andiko; Parliament and Accountability in East Africa ambapo ameweza kuangalia mhimili wa Bunge katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki yaani kuchambua kwa kina na hata kufanya ulinganifu wa Bunge la Tanzania, Kenya, na Uganda.

Napenda vitabu ambavyo kutokana na kuvisoma vinakusukuma kusoma vitabu vingine zaidi na zaidi. Tawasifu ya Jaji Steven Bwana ilinisukuma kusoma kitabu cha Jaji Barnabas Samatta; Uhuru wa Mahakama. Ni kitabu ambacho kinatoa ufahamu mpana wa namna Mahakama zetu zinafanya kazi. Changamoto zinazokabiliana nazo hasa katika jukumu la kusimamia haki.

Jenerali Twaha Ulimwengu, moja ya magwiji ninaowahusudu hasa kwa uwezo wake mkubwa kuchambua na kueleza mambo. Mwaka huu, 2021 alitubariki kwa mkusanyo wa makala zake za nyuma; Rai ya Jenerali Ulimwengu-Juzuu III. Nimemudu kukisoma tena makala ambazo alikwisha aandika na baadhi zingalizinaishi hata leo. Ni kitabu kizuri na muhimu kwa wapenzi wa siasa, utawala bora, kuandika. Ni muhimu hasa kwa kizazi cha leo kufahamu tulipotoka, tulipo ili kuweza kujipanga vyema katika kesho yetu. Kitabu hiki ni moja ya ufunguo huo.

Mwisho ningependa kuhitimisha kwa vitabu viwili vya riwaya za kisiasa ambavyo nilivisoma; The Wizard on the crow cha Ngugi wa Thiongo na Chochoro za Madaraka cha Lello Mmassy. Ugwiji wa Ngugi sina haja kuzama kumjadili bali niliguswa sana na maudhui ya kitabu hasa kwa yale ambayo nchi yetu ilikuwa ikiyapitia kwa miaka mitano na miezi mitatu nyuma ndipo nikasukumwa kukisoma. Namna baadhi ya wanasiasa hata wa ngazi ya juu kama Mawaziri wetu walivyokuwa wakienenda bila kuwasahau wasomi. Nikija kwa kitabu cha Chochoro za madaraka; Mmassy ameendelea kujaribu kusadifu maisha katika nafasi za juu za uongozi wa nchi na namna ambavyo nchi kubwa zenye nguvu zinahusika katika maamuzi ya kiuongozi.

Kwa muhtasari orodha ya vitabu ni kama ifuatavyo;
1. The Wave: Migraineur memoir-Rahma Bajun
2. Maisha yangu, Utumishi wangu-Steven James Bwana
3. Uhuru wa Mahakama-Jaji Barnabas Samatta
4. Mzee Rukhsa-Ali Hassan Mwinyi
5. Biubwa A. Zahor- Zuhura Yunus
6. Niliyoyashuhudia Jela-Mohamed Majaliwa
7. The President’s Keepers-Jacques Pauw
8. In the footsteps of Mr. Kurts-Michela Wrong
9. Selous, The lost Sanctity-Attilio Tagalile
10. John Magufuli; an epitome of cowardice- Ansbert Ngurumo
11. The Second Mountain-David Brooks
12. Argument: a guide to critical thinking- Perry Weddle
13. Parliament and Accountability in East Africa-Tundu Lissu
14. Rai ya Jenerali Ulimwengu-Juzuu III-Jenerali Twaha Ulimwengu
15. Chochoro za madaraka- Lello Mmassy
16. The Wizard on the crow-Ngugi wa Thiongo

--

--

Michael Dalali

"Truth is an inseparable companion of justice and mercy"-@pontifex| Cogito Ergo Sum| Analyst| Strategist| Facilitator| Translator| Writer & Avid Reader! 🥋