Michael Dalali
7 min readDec 31, 2018

Vitabu vilivyonijenga mwaka 2018!

Tunapoelekea kuumaliza mwaka huu, 2018 kama ilivyo ada napenda kuwashirikisha vitabu ambavyo nimemudu kuvisoma.

Naamini kwa kufanya hivi-itakuwa sehemu ya chachu ktk kuamsha na kuimarisha ari ya usomaji vitabu na si vinginevyo mintarafu kujikoga au kuringishia.

Kwa mwaka 2018 nimesoma kikamilifu jumla ya vitabu 18 kulinganisha ilivyokuwa kwa mwaka jana, 2017 ambapo nilisoma vitabu 17.

Orodha hii haitaweka vitabu ambavyo nilianza kuvisoma na kuishia katikati ya njia.

Katika kundi la Falsafa nimesoma vitabu viwili;

  1. Power-Bertrand Russell [Russell ni moja ya waandishi wa Falsafa ambao napenda sana maandiko yake]

2. The Emperor’s Handbook: Marcus Aurelius-C. Scot Hicks and Davis V. Hicks [Huwa namhusudu sana Marcus Aurelius kwa falsafa na mafundisho yake “stoicism”].

Ukiacha kundi la Falsafa, pia kuna kitabu ambacho mwandishi amekiandika akiwa ameshawishiwa na kutengenezwa fikra kwa mtindo wa falsafa za kistoiki (stoicism), ambazo nami nazihusudu;

3. Ego-Ryan Holiday [Hiki ni kitabu kimeandikwa vizuri sana na Ryan hasa kumsaidia mtu yeyote kujiepusha na kiburi (Ego). Na namna gani kiburi ni hatari ktk ustawi. Pia namna gani kwa kupitia falsafa za kistoiki mtu anaweza kuenenda vyema na kuishi vyema na watu. Namshukuru rafiki yangu, Ramadhani Msoma kuniazima kitabu hiki].

Kwenye eneo la siasa, nimejikuta nimesoma vitabu ambavyo vimejikita katika siasa ya India na wanasiasa wa India. Kwa muda sasa nimekuwa nafatilia siasa ya India, kuna mengi ya kujifunza;

4. Half Lion: How P.V. Narasimha Rao transformed India-Vinay Sitapati [Half Lion, ni kitabu nimekifurahia sana-kimeweza kusafiri ktk maeneo kama uchumi, siasa ngumu za matabaka na koo zenye kuhodhi siasa nk. Waziri Mkuu Rao ni moja ya mhimili muhimu wa India ya sasa tunayoiona. Na ni mwanasiasa ambaye amemudu kuwaibua wanasiasa wengine toka ktk taaluma zao na kuwafanya wanasiasa hadi baadae wakashika nyadhifa za juu kabisa kama Waziri Mkuu M. Singh na wengine]

5. Sonia Gandhi-Rani Singh [Hiki pia ni kitabu kizuri nilifurahia sana, kimeweza kuchambua kwa kina maisha ya Mama Sonia Gandhi na namna gani siasa za koo zilivyo na yepi huwa wanapitia. Pia kwa kitabu hiki, unaweza kuona. namna gani koo zinazohodhi siasa zilivyo na mchango mkubwa karne hata karne sambamba na namna gani wanajiandaa na kuhakikisha wanaendelea kuhodhi].

Tukibaki ktk nchi ya India. Nimesoma kitabu cha;

6.The Gift-Arun Gandhi. [Kitabu hiki ambacho kimejikita katika mafunzo ya Mahatma Gandhi ambayo yameandikwa vyema na mjukuu wa Gandhi. Mafunzo muhimu kama; unyenyekevu, kusimamia kweli, mapambano pasina mapigano, kujitesa mwili kama sadaka nk. Kwa namna ya kipekee namshukuru Shemeji yangu, Brighita Faustine kwa zawadi hii]

Nilifurahi sana niliposikia habari ya aliyekuwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mzee Ludovick Utouh kuandika kitabu cha maisha yake;

7. Kalamu isiyokuwa na wino-Ludovick Utouh [Ni kitabu kimeandikwa vizuri na kimemudu angalau kwa uchache wake kuweza kuweka kumbukumbu ya baadhi ya kazi na jitihada ktk kuhakikisha Serikali na nchi inasimamia uwajibikaji na kuhakikisha uwazi katika matumizi ya umma. Kimeweza kuainisha vizuri pia haja ya uwezo wa Kamati za bunge imara ili taifa liwe la uwajibikaji].

Kuna nyakati ambazo vitabu vigumu vinakuwa havipandi kutokana na akili kuchoka na pia hekaheka za majukumu, basi hapo riwaya zinakuwa muafaka kupoza akili;

8. The thing around your neck-Chimamanda Ngozi [Ni kitabu nilikifurahia pia kwa kuleta hadithi fupi fupi katika kitabu kimoja. Ni mtindo mzuri wa kiuandishi]

9. Why I Write-George Orwell [kitabu hiki kimeandikwa miaka mingi nyuma ila bado kinaishi. Kimesanifu siasa, uandishi nk. Namshukuru rafiki yangu, Francis Sampa kwa kuniazima kitabu hiki]

Waandishi wa ndani, nao hawakuwa nyuma. Niliweza kusoma kazi nne za riwaya ambazo hakika nilizifurahia;

10. Upako toka kuzimu-MM.Mwanakijiji [Hiki namshukuru Pd. Paul Raia kwa kunihamasisha kukisoma. Niliweza kusafiri ktk yale ambayo yanatokea hasa kwa mwandishi kuandika juu ya yanayojiri katika baadhi ya Makanisa]

11. Broken Heart-Shishi na Futa [awali niliposikia habari ya hiki kitabu sikuwahi kufikiri ningekuja kukisoma. Hata pale nilipokikuta nyumbani bado sikuona kama ni aina ya mwandishi ninayepaswa kusoma. Ila nilipofungua nilivutiwa na ubora wa hali ya juu ya karatasi, uchapaji uliokuwa ktk kitabu. Nikaanza kusoma sura ya kwanza….la haula, kitabu hakikuwekeka chini mpaka nilipomaliza. Kilikuwa kizuri sana. Heko kwako Futa kwa kazi nzuri. Kilichonikera tu kimoja; mhusika mkuu alidumu kutuambia ana siri ya yaliyomkuta akiwa Sekondari, kila sura nk akirejea bila kuielezea mpaka kitabu kikaisha pasina kuitaja].

12. Mtoto wa Mama- Adam Shafi [Mzee Shafi ni moja ya manguli ktk uandishi wa riwaya nchini. Nami humhusudu sana kwa kazi zake. Nilipoona tu kitabu chake kipya niliwahi kukinunua. Ni kitabu kizuri sana ila sio “wow”! Si viwango vyake Mzee Adam Shafi hasa kama umeshasoma kazi zake zingine za awali. Kuna kitu kimepungua ktk uandishi].

13. Mtafiti-Hussein Tuwa [Jina la Hussein Tuwa ni jina kubwa sana pia ktk waandishi wa kizazi cha sasa. Nimekuwa nasoma kazi zake na kufurahia sana. Kazi ya Mtafiti ilikuwa nzuri. Ingawa mwe, matumizi ya neno “Wakha” nadhani yalivuka viwango, mwandishi alilitumia neno hilo mno mpaka ikafika hatua unafahamu ikiisha sentensi moja baada ya mbili lazima ukutane tena na neno “wakha”. Shukran kwa Jestina Kimbesa kuhakikisha napata nakala].

Katika eneo la kiroho, niliweza kusoma jumla ya vitabu vitano. Vipo vingine ambavyo kwa ukubwa wake bado naendelea kuvisoma [hasa Summa Theologiae cha Mt.Thomas Aquina na Omnibus of sources cha Mt. Fransisko wa Asizi];

14. Power of Silence-Robert Cardinal Sarah [Ni moja ya kitabu nilikipenda na kujifunza mengi mno toka kwa Baba Kardinali Robert Sarah. Kuanzia umuhimu wa sala, kutenga muda wa unyamavu nk…niliandika makala kadhaa kutokana na mafundisho ndani ya kitabu hiki. Ni kitabu ambacho namshawishi mtu yeyote mwenye kuhitaji ukaribu na Mungu kukisoma]

15. GOD or Nothing-Rober Cardinal Sarah [Baada kusoma Kardinali Robert Sarah kwenye kitabu chake “Power of Silence” kikanisukuma kusoma maandiko yake mengine. Hiki ameweza kuandika vyema historia yake. Ni kitabu muhimu sana kusomwa na watumishi wa Mungu ambao wamejitoa maisha yao hasa nyakati hizi zetu za sasa ambazo tunaamini uhuru unabinywa na kila mtu anaguswa kwa wakati wake. Alipitia madhila makali nchini Guinea chini ya Dikteta Sèkou Tourè. Na nilishtushwa kwa namna Sèkou Tourè alivyoelezwa mwisho wake alivyogeuka dikteta tofauti na ambayo nilikuwa namjua kadiri ya mafundisho ya historia shuleni. Padre, Mchungaji, Askofu, Sheikh nk kitawafaa sana kukisoma hiki!]

16. Pray the rosary like never before-Edward Sri [Edward ameweza kuchambua kwa kina umuhimu wa rozari takatifu. Amehamasisha na alinigusa mno juu ya haja ya kusali rozari kila siku].

17. Humility Rules- J. Augustine Wetta, OSB [moja ya kitabu kizuri sana kilichoandikwa kwa lugha nyepesi kuelezea mafundisho ya Baba Abate Benedikto ktk msingi wa andiko lake kwa shirika la Mabenediktini; “Rules”

18. Fahamu mambo 40 ya Misa Takatifu-Pd. Stefano Kaombe [Hiki naweza kusema ni kitabu funga dimba kwa mwaka huu. Ni kitabu kizuri sana na kimeandikwa na mwandishi ninayemhusudu sana kwa karama yake ya uandishi. Itoshe kusema-ni kitabu muhimu sana kwa kila Mkatoliki kuhakikisha anakisoma ili aweze kushiriki kikamilifu pasina makosa Misa Takatifu].

Kwa neema ya Mungu, kitabu ambacho ninaingia nacho mwaka 2019 ni cha siasa za India kikiwa kimeandikwa na Waziri Mkuu wa kwanza wa India, Jawaharlal Nehru; Discovery of India. Pia natazamia kusoma vitabu vifuatavyo mapema mwakani;

  • Let her fly-Ziauddin Yousafzai [Baba wa Malala na namna gani amechangia ktk mapambano ya kuhakikisha usawa na haki za mtoto wa kike ktk mazingira magumu ya jamii ya Pakistan]
  • Becoming cha Michelle Obama [hiki sina haja ya kusema mengi 😜]

Kwa neema za Mungu, na nikiwa na “mood nzuri” (maana uandishi wangu huathiriwa sana na “mood”) bila shaka nitamaliza viporo vyangu viwili vya miswada;

Mosi, Mang’amuzi yangu juu ya mafundisho ya Kanisa Katoliki [Hiki ni uvivu tu maana kipo robo tatu tayari bado robo tu kuimalizia]

Pili; riwaya ya kisiasa!

Michael Dalali

"Truth is an inseparable companion of justice and mercy"-@pontifex| Cogito Ergo Sum| Analyst| Strategist| Facilitator| Translator| Writer & Avid Reader! 🥋